Hospitali ya Muhimbili imethibitisha kuwa, majeruhi 3 kati ya 11 wa ajali ya moto Morogoro waliokuwa wamelazwa Hospitalini hapo, wameruhusiwa kurudi nyumbani baada ya afya zao kuimarika.

Akizungumza leo Septemba 12, Dkt Edwin Mrema  ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Upasuaji amesema kuwa, kabla ya kuwaruhusu  hospitali hiyo imewapa huduma za kisaikolojia kwa kuwa tatizo la moto lilikuwa limewathiri kwa kiasi kikubwa.

“Mgonjwa ambaye hadi sasa yuko ICU, kuwa alikuwa ameungua zaidi miguuni, iliwalazimu kutoa viungo ambavyo vilionekana kupoteza uhai na amehifadhiwa katika chumba maalumu cha uangalizi ili kuzuia maambukizi kwa majeraha yake” Amesema Dkt Mrema .

Aidha wakati mgonjwa mmoja bado yupo ICU, wengine wapo wodi ya kawaida wakiendelea na matibabu na hali zao zinaimarika.

Tukio la ajali ya moto Mkoani Morogoro, lilitokea siku ya Agosti 10, baada ya Lori la mafuta kupinduka na kupelekea mlipuko huo ulioua zaidi ya watu 60 papo hapo, ambapo hadi sasa vifo vya ajali ya moto huo viko 104.