Mfalme wa vichekesho nchini Amri Athuman maarufu kama Mzee Majuto ameacha wosia kwa watoto wake siku moja kabla ya kufariki dunia.

Akizungumza leo Ijumaa Agosti 10, 2018 mtoto wa marehemu, Hamza Athumani aligusia wosia huo wakati akisoma wasifu wa baba yake.

Amesema Agosti 7, 2018 alikwenda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kumjulia hali Majuto aliyekuwa amelazwa, akiwa ameambatana na rais wa shirikisho la filamu, Simon Mwakifamba na Majuto kuwaeleza kuwa wote ni watoto wake na kutaka wapendane, wasibaguane katika kila jambo.

Hamza amesema kufuatia maneno hayo ya baba yake, aliwaomba ndugu zake kuyazingatia. Majuto alifariki dunia Agosti 8, 2018 saa 2 usiku.

“Ndugu zangu nawaita mara tatu nawaomba tufuate wosia wa baba aliotuachia, amesema tupendane tusaidiane na wote ni watoto wake,” amesema Hamza akiwataka ndugu zake hao kutosikiliza maneno ya nje kuhusu inavyosemwa familia ya mfalme huyo wa vichekesho.

Amesema Mzee Majuto ameacha watoto 10 na kwamba walikuwa 15 lakini watano walifariki dunia.