Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewataka viongozi wa dini ya kiislamu nchini kuunga mkono vita ya matumizi, uingizaji na usafirishaji wa dawa za kulevya kutokana na athari kubwa zinazojitokeza kwa vijana.

Akizungumza katika semina ya viongozi wa dini ya kiislamu, wakiwemo mashekhe, Maimam pamoja na walimu wa Quran, Makonda amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano kupitia vyombo vya dola kuwakamata na kuwahoji baadhi yao wamekuwa wakidhihaki vita hivyo.

“Unga hapa mjini sasa umeadimika mashekhe wangu, hata bei umepanda na wanaouza sasa hivi hawauzi kama njugu, sasa hivi wanauza kwa kujificha. Lakini sisi tumeamua kuongeza kasi na wale wote waliotajwa majina yao yanasambazwa airport kona zote kama ni boda ili wawatambue. Sasa ukiwagusa watu wenye pesa mtikisiko lazima uwepo, na ndio maana wakati natangaza mara ya kwanza niliwaambia hizi ni rasha rasha wa pili nikawaambia huu utakuwa mgumu kidogo bado ya 3 watu ooh wanapiga kelele sasa 4,5 6 na 7 huko ndio kuna balaa,” alisema.

Aidha mkuu wa mkoa alisema vita hiyo haitamuonea mtu yeyote isipokuwa vitazingatia sheria pale mtu atakapotiliwa mashaka atahojiwa na watakaobainika majina yao yatapelekwa kwenye vyombo vya usalama ili watiwe mbaroni.