Mama mmoja mdogo nchini China ameamua kuuza maziwa yake mwenyewe ya kumnyonyesha mwanae ili kuweza kupata fedha itakayomsaidia kulipia gharama za hospitali kwa ajili ya binti yake mgonjwa.

Katika video ambayo imekuwa ikionekana katika mitandao ya kijamii, mama na baba wa mtoto huyo mgonjwa wanaeleza kuwa wanahitaji kukusanya fedha zipatazo yuan 100,000 ambazo ni sawa na dola 1600 kwa ajili ya mtoto wao ambaye yuko katika chumba cha mahututi akipata matibabu.

Video hiyo ambayo imetazamwa na zaidi ya watu milioni 2.4 na imejibiwa na watu 5000 tangu ilipowekwa kwenye mitandao ya kijamii ya huko nchini China.

Video hiyo iliyopigwa katika eneo la kuchezea watoto lijulikanalo kwa jina la Shenzhen katika mji wa jimbo la Guangdong huko China.

Mama anayeuza maziwa yake ya kunyonyesha ili kupata fedha za haraka kwa sababu pacha mmoja wa watoto wake wa kike yuko katika chumba cha mahututi katika hospitali ya Bao’an.Huku mume wake akieleza kuwa hospitali wanawadai zaidi ya dola 1600.

Aidha kumekuwa na malalamiko juu ya mpango wa afya nchini China kwa kudai kuwa vituo vya afya vimekuwa na usumbufu katika kupata huduma na watu kuhitajika kulipa zaidi ili wasipange foleni.

Majibu ambayo yameandikwa katika mtandao mengi yameonekana kuwa ya kuwaonea simanzi huku wengine wakiendelea kushirikisha wengine kwa kuandika maneno haya,“uza maziwa ,kumuokoa binti”

wazazi
Wazazi wakiwa barabarani nchini China wakiomba msaada kwa ajili ya mtoto wao mgonjwa

Ingawa wengine wakiwataka wapita njia wawape fedha huku wengine wakidai kuwa watajitolea kuwapa msaada kama watawaona wazazi hao barabarani.

Na kuna mtu aliweka maelezo yaliyopendwa na zaidi ya watu 3000, yanayosema Pale mtu wa hali ya chini katika jamii anapougua sana, huwa anakosa hata haki zake muhimu.

Lakini kuna wengine wachache ambao waliona jambo la kuuza maziwa yake ni utaratibu mbaya wa kuomba msaada.

Mwingine alisema ,Kila mtu anaweza kuelewa kuwa hawana uwezo na wanatumaini kuwa watapata msaada, lakini kwa nini wanaondoa utu wao kwa kuuza maziwa .

Mtu mwingine alikosoa maelezo yaliyokuwa yanakashfu maamuzi ya wazazi hao na kudai kuwa huo ni upendo wa dhati wa wazazi ambao hawajiwezi kabisa, hivyo hao wanaotoa maneno mabaya juu yao kwenye mitandao wanapaswa kujifikiria kama ingekuwa ni mtoto wao, wangejali muonekano wao au maisha ya mtoto wao.