Aliyekuwa ‘scout’ wa klabu ya Chelsea, Daniel Boga amesema kuwa mama mzazi wa nyota wa Paris Saint-Germain, Kylian Mbappe ndiye aliyesababisha kinda huyo kuondoka Stamford Bridge mwaka 2012.

Mfaransa huyo, Mbappe amewahi kufanya majaribio ‘the Blues’ akiwa na umri wa miaka 13 na kuitumikia timu ya vijana ili kuendelea kuonyesha uwezo zaidi.

Lakini kwa mujibu wa Boga, klabu hiyo ya ligi kuu England haikuvutiwa na kiwango alichokionyesha na hivyo kumuomba kurudi kwa awamu nyingine kwaajili ya majaribio lakini, Fayza Lamari ambaye ni mama mzazi wa mchezaji huyo akakataa.

”Nilimleta yeye na familia yake, alikuwa mwenye ujuzi kama aliyo nao hivi sasa na alicheza dhidi ya Charlton na kushinda mabao 7 – 0,” amesema Boga.

Boga ameongeza ”Katika ile wiki yake akiwa Chelsea, tulikwenda ofisini na kumuambia tumekiona kipaji chake lakini tunakualika urudi tena kwa mara nyingine ujekufanyiwa majaribio na baada ya hapo tutajua chakufanya,”.

”Nakumbuka ile siku mama mzazi wa Mbappe alisema kwa Kifaransana nikajaribu kutafsri kwa lugha ya Kiingereza, ambapo aliniambia, sikiliza kijana wangu hawezi kurudi na kama mnamuhitaji mnalazimika kumchukua sasa miaka mitano ijayo itawagharimu euro milioni 50 kumnunua.”

Boga ambaye alilazimika kutafsri alichozungumza, Fayza amesema kuwa licha ya kijana huyo kuonyesha kiwango cha hali ya juu, katika soka la England kwa wakati huo lilikuwa likihitaji wachezaji wanaotumia nguvu na juhudi kitu ambacho Mbappe alikuwa hana hivyo kumpatia muda mwingine wa kuja kwa majaribio ili kuona namna ya kuboresha uwezo wake.