Mamlaka ya mafunzo ya amali Zanzibar imewataka vijana wanaomaliza skuli na kushindwa kuendelea na masomo yao kujiunga na vituo vya mafunzo ya amali ili kujiendeleza kwa kazi mbalimbali za ufundi na ujasiriamali.

Akizungumza na mwadishi wa habari hizi Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo Bakari Ali Silima amesema vyuo vya amali ni sehemu ya kujiendeleza kimaisha kutokana na taaluma inayotolewa katika vyuo hivyo kwa kuwafanya vijana kuwa na uwezo na kujipatia ajira kwa urahisi au kujiajiri wenyewe.

Amesema vipo vituo vingi vinavyotoa taaluma au mafunzo hayo lakini idadi ya watu wanaojitokeza kujiunga kwa ajili ya kupata ujuzi huo bado hairidhishi.

Amefahamisha kuwa serikali imenunua vifaa mbali mbali vya kufundishia na kujenga uwezo wa kufanya kazi kwa wananchi pamoja na kuendeleza ujenzi wa vituo hivyo.

Aidha ametoa wito kwa vijana wa mkoa wa kaskazini na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi ili kupata ujuzi utakaowasaidia katika maisha yao.