Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Mh. Hassan Khatib Hassan amezitaka mamlaka za kisheria nchini kutoa taaluma kwa wananchi kila kunapotokea mabadiliko ya sheria mbali mbali ili waweze kuzitambua na kuepukana na makosa yasio ya lazima.

Mh. Khatib ametoa kauli hiyo ofisini kwake Tunguu katika kikao cha pamoja kilichozungumzia juu ya marekebisho ya sheria ya kikosi maalum cha kuzuwia magendo nam i ya mwaka 2003 kwa maofisa kutoka taasisi za serikali zinazohusiana na magendo ikiwemo KMKM, ZMA, ZRB, Afisi ya Mkurugenzi wa mashtaka na jeshi la polisi.

Amesema licha ya Serikali kuendelea na jitihada za kuzifanyia marekebisho sheria mbali mbali za nchi lakini bado wananchi walio wengi hawana uwelewa juu ya marekebisho ya sheria hizo jambo ambalo linapelekea kuendelea kufanyika kwa makosa mbali mbali pasi na kutambua.

Akifafanua juu ya sheria hiyo mpya ya magendo ambayo imeshaanza kutumika nchini mwanasheria kutoka kikosi cha kuzuwia magendo ndugu Ismail Andrew Karya amesema urekebishwaji wa sheria hio imeipa uwezo mkubwa kikosi hicho juu ya ufanikishaji wa majukumu katika suala zima la kupambana na biashara ya magendo.

Nao wakichangia juu sheria hiyo mpya washiriki katika kikao hicho kutoka mamlaka husika wamesema  mashirikiano pamoja na uadilifu unahitajika ili kuweza kutekeleza vyema sheria hiyo ili kuondosha kabisa tatizo hilo.

 

Na: Rauhiya Mussa