Raia wa Marekani leo wanapiga kura ya kumchagua Rais atakayeliongoza taifa hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Mwaka huu kama ilivyo kwa kila baada ya miaka minne raia wa Taifa la Marekani wanaingia katika uchaguzi wa nafasi ya urais.

Katika uchaguzi huo Mgombea DONALD TRUMP wa chama cha Republican atachuana dhidi ya mgombea wa chama cha Democratic HILLARY CLINTON.

Nguvu zote zinazotumika kwa wananchi wa Marekani duniani kote kuhamasishwa kupiga kura mapema au kupiga kura kisha kutuma kwa njia ya posta lakini ukweli ni kwamba kura zao sio zinazoamua nani awe Rais bali kikundi cha watu ndio kinaamua, kikundi hicho kinaitwa Electoral college.

Kuelewa kuhusu Electoral College inabidi kurudi kidogo katika historia ya taifa hili.  Marekani ina  majimbo 50 na ukijumlisha na Washington DC katika muktadha wa mchakato wa uchaguzi yanahesabika kuwa 51.

Majimbo haya yanatofautiana kwa ukubwa na wingi wa watu. Katika kuleta uwiano na kuhakikisha Rais wa Marekani hajikiti katika majimbo yenye watu wengi pekee, waasisi wa taifa hili waliamua kuwe na wapigaji kura maalum wanaochaguliwa na vyama vyao ambapo wanatokana na ukubwa wa majimbo mfano WISCONSIN kura ni 10, jimbo la IOWA kura sita  huku jimbo la  California likiwa na kura 55.

Kwa hiyo kundi la watu 538 ndio wanaoamua nani awe rais wa Marekani  kwahiyo wamarekani wanavyokwenda kupiga kura wanawapigia kura hawa wawakilishi wao ambao mara nyingi wanakuwa ni makada wa vyama vyao.

Baada ya wananchi wa Marekani kupiga kura jumanne tarehe 8 novemba , kura zao zinahesabiwa na mgombea mmoja atakayeongoza kura hizo maana yake ni kuwa  chama hicho kitachukua kura zote za jimbo hilo. Hii inamaanisha kuwa mgombea ambaye atafanikiwa kufikisha kura 270 ndio atakuwa mshindi wa urais.

Pengine unaweza kujiuliza kwanini wagombea wengi hapa wanatumia nguvu nyingi kushawishi mashabiki wao kupiga kura katika majimbo mbalimbali?

Hii ni kutokana kuwa kuna majimbo ambayo yamekuwa yakijulikana ni ya chama  fulani lakini kuna majimbo ambayo yamekuwa yakibadilika badilika majimbo hayo yanaitwa swing states na ndiyo wagombea DONALD TRUMP na HILLARY CLINTON wamekuwa wakitumia nguvu kubwa kushawishi wapiga kura kuzipata kura zao.

Kwa kifupi , wananchi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi ni kwa kuwa wanavyopiga kura wanachagua wawakilishi wao na wakishinda kuwa wengi maana yake ni kura nyingi na hivyo kushinda jimbo hilo , … na kura nyingi maana yake ni ushindi kwa mgombea wao ambaye licha ya ushindi wake kufahamika Novemba hii, atatangazwa rasmi Januari 20 ya mwaka  2017 kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi.

11