Mashindano ya Afrika Mashariki ya mpira wa mikono yanayofanyika Zanzibar yanatarajiwa kunza rasmi Jumapili Novemba 11, 2018 kwenye viwanja vya Jeshi Nyuki ambapo jumla ya vilabu 16 vinatarajiwa kushiriki mashindano hayo.

Akizugumza na vyombo vya habari kwenye ukumbi wa BMTZ  Visiwani hapa Mwenyekiti wa chama cha mpira wa mikono Zanzibar (ZAHA) Salum Hassan Salum amesema kwa sasa hatua iliyofikiwa ni kuwapokea wageni kutoka nchi mbali mbali za Afrika Mashariki ikiwemo DRC Congo ambao watakuja na timu nne na Kenya timu 6.

Aidha amesema ZAHA imeshajindaa kama viongozi kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika ikiwa baadhi ya nchi bado zinasuasua kushiriki kuleta vilabu vyao ikiwemo Rwanda, kwa upande wa gharama wao kama ZAHA wanabeba gharama za usafiri na malazi baadhi ya gharama zinakuwa chini ya Shirikisho la mpira wa mikono Afrika (CAHB).

Aidha amesema mashindano hayo wanatarajia kuhudhuriwa na Raisi wa Shirikisho la mchezo huo Afrika (CAHB) kutoka Benin akiambatana na wageni wengine kutoka nchi mbali mbali za kanda ya Afrika Mashariki na kati.

Kwa upande mwengine amesema mashindano hayo yanatarajiwa kuendana na kozi maalum ya waamuzi na kozi za makocha wa mchezo huo zitakazo ratibiwa na shirikisho la mpira wa mikono Duniani (IHF) zitaratibiwa na Katibu wa Shirikisho la Mpira wa mikono Afrika Mashariki Charles Omondi Oduo na Geremi kutoka Cameroon.

Kwa upande wa ratiba ya mashindano hayo amesema itajulikana baada ya kamati tendaji  kukutana baada ya wajumbe wote kutoka nchi za Afrika Mashariki kukutana na kuamua namna ya upangaji wa ratiba hiyo.

Kwa upande wake katibu mkuu wa ZAHA Mussa Abdurabil Fadhil amesema kwa upande wa Zanzibar jumla ya vilabu viwili vimethibitisha kushiriki mashindano hayo navyo ni Nyuki na JKU lakini bado ni changamoto kubwa vilabu vyao na bado vinanafasi ya kuomba ushiriki wa mashindano hayo.

‘’Nawaomba sana wafanya biashara hii ni fursa pekee kwa Zanzibar wanaweza kuja kuwekeza kwenye mashindano haya makubwa kwa kanda yetu ya Afrika Mashariki na kati’’ Alimalizia Mussa Abdurabil Fadhil…..