Mkurugenzi Mtendaji Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa  Zanzibar Makame Khatib Makame amesema ili kukabiliana na  maafa  ni vyema kuunganisha nguvu za pamoja kwa Wadau mbalimbali nchini ili kupunguza athari zinazoikumba jamii.

Akizungumza katika kikao cha kujadili Muongozo wa kukabiliana na Maafa Zanzibar huko Maruhubi alisema endapo Wadau wataunganisha nguvu za pamoja katika mipango na mikakati kupitia sera ya maafa itasaidia kupunguza athari za maafa nchini.

Alisema muongozo huo utawasaidia watu wenye mahitaji maalum, watoto na watu wazima kupata elimu ya kukabiliana na maafa ili waweze kujikinga,kukabiliana na kurejesha hali baada ya maafa kutokea.

Hata hivyo aliwataka Masheha pamoja na Kamati za Maafa kuendeleza na kusimamia mikakati ya kutoa elimu ya kukabiliana na maafa iliowekwa ili  kuiwezesha jamii ipate uwelewa wa kujihami na kujilinda endapo maafa yakitokea .

Nae Mshauri  Muelekezi wa Muongozo huo kutoka Maahad Istiqama Tunguu  kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) Mussa  Juma Mzee alisema jamii ifahamu njia bora ya kukabiliana na maafa na majanga ya kimaumbile na ya kusababishwa na binaadamu.

Alifahamisha muongozo huo utaweza kutoa mbinu za ufundishaji na  kujuwa jinsi ya ufahamu kwa waliofundishwa .

“lengo ni kuwa na utaratibu ambao utawasaidia Mfundishaji na Mfundishwaji kwenda sambamba katika kufahamiana  ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,”alisema Mshauri huyo.

Alieleza jamii itaweza kujitoa katika mazingira ya hali ya hatari pindipo watapopewa mafunzo ya kujiepusha na athari zitazosababisha maafa katika shughuli zao na mazingira yanayowazunguka.

Alifahamisha kuwa jamii bado uwelewa wao ni mdogo kutokana na maafa hivyo iko haja ya kuelimishwa hatua ya awali ya kuweza kuripoti mara tu baada ya maafa kutokea ili aweze kupatiwa msaada wa haraka.

Nao washiriki wa Kikao hicho wamesema muongozo huu  utawaelekeza jinsi ya kutoa elimu kwa watendaji wao na  katika  sekta zao. 

Story na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar