Matawi ya Simba SC mkoani Lindi yamepanga kuchangia maandalizi ya timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye  Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (TPL)  na Ligi ya Mabingwa  Barani Afrika (CAFCL) ya msimu ujao.

Hayo yamelezwa wakati wa hafla ya kuipongeza timu ya Simba SC kufikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa  Barani Afrika. Hafla ambayo ilifanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Lindi View Resort, iliyopo katika manispaa ya Lindi.

Akizungumza kwaniaba ya matawi ya Mchinga, Nachunyu, Kitomanga na Mitwero ambayo yalituma wawakilishi  kwenye hafla hiyo. Mwenyekiti wa tawi la Mshikamano, Salum Fundi alisema wameamua kuchangia maandalizi ya timu hiyo itakapo kuwa kambini wakati inajiandaa kwa msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Fundi alisema wanajua kwamba Simba ni klabu ya wanachama na licha yakuwa na mwekezaji mwenye asilimia 51 ya hisa, bado wana wanawajibu wa kuchangia ili kumtia nguvu mwekezaji huyo ambaye amesababisha timu hiyo kufikia hatua hiyo kubwa Afrika.