Taarifa za kisa cha mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno zimetawala vichwa vya habari nchini Kenya, kila siku kukitokea jipya kuhusu mauaji hayo.

Bi Otieno alikuwa ametekwa pamoja na mwanahabari wa shirika la Nation Media Group Barrack Oduor kabla ya mwili wake kupatikana ukiwa umetupwa vichakani Oyugis katika jimbo la Homa Bay.

Mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Sharon Otieno alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Rongo, ambapo alikuwa anasomea shahada ya sayansi ya habari na stakabadhi za kitabibu katika chuo hicho.

Alikuwa na ujauzito wa miezi saba na taarifa zinasema alikuwa ameamua kuahirisha masomo yake kwa muda.

Ni mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 26 na alikuwa ameolewa awali na mwanamume kwa jina Bernard Okuta.

Sharon Otieno

Sharon Otieno alikuwa na mimba ya miezi saba

Msemaji wa familia ya Sharon Joshua Okong’o anasema Okuta ni mwalimu wa shule ya upili na wawili hao walikuwa wamejaliwa watoto watatu, mmoja wa kiume na mabinti wawili.

Awali, wawili hao walikuwa wanaishi katika moja ya nyumba za shule ya upili ya Rapogi katika kaunti ya Migori ambapo Okuta amekuwa mwalimu kwa miaka minne unusu. Hata hivyo wanadaiwa kutengana mwaka jana ambapo Sharon alihamia nyumbani kwa wazazi wake Homa Bay.

Sharon anadaiwa kukutanishwa na mwandishi Barrack Oduor na diwani wa zamani wa eneo la Kanyandoto, Homa Bay Lawrence Mula ambaye alimfahamisha kwamba alikuwa na rafiki yake aliyetaka usaidizi wake kama mwanahabari.

Ni siku hiyo ambapo Sharon alikutana mara ya kwanza na Oduor ambapo alimwambia kwamba Gavana wa Migori Okoth Obado alikuwa amemtelekeza baada yake kubeba mimba yake.

Sharon alimwambia mwandishi huyo kwamba awali alikuwa anaweza kupata kiasi chochote cha pesa alizotaka kutoka kwa gavana huyo. Mwanamke huyo alikuwa na kanda ya sauti aliyomchezea mwandishi huyo ambapo mwanamume anayedaiwa kuwa gavana huyo anasikika akijaribu kumshawishi atoe mimba yake.

Oduor anasema baadaye alipigiwa simu na mtu aliyejidai kuwa gavana huyo, ambaye hakutaka kukiri wala kukanusa madai hayo.

Gavana huyo alimwambia kwamba mwanamke huyo alikata kumsaliti na kumtishia kwamba angefichua siri kuhusu mimba hiyo ili kujifaidi. Alimwambia Oduor kwamba baada ya hapo angeendeleza mawasiliano na msaidizi wake Michael Oyamo.

Sharon baadaye anadaiwa kumwambia mwandishi huyo kwamba gavana kupitia Oyamo alitaka kukutana na wawili hao mnamo tarehe 4 Septemba majira ya jioni.

Migori

Sharon na Oduor walikuwa wamekutana eneo la Rodi Kopany ambapo awali walikuwa na miadi lakini Oyamo alimfahamisha Sharon kwamba mkutano ulikuwa umebadilishwa hadi mjini Rongo.

Walikwenda Rongo ambapo Oduor alipendekeza wakutane katika mgahawa ufahamikao kama Graca, wakaingia na kuketi. Oyamo anadaiwa kumpigia Sharon simu kuthibitisha kwamba Oduor alikuwepo. Baadaye Oyamo akafika akaingia msalani na alipotoka akapendekeza wahamie pahala pengine.

Watatu hao waliondoka kwa pamoja na hapo nje kulikuwa na gari jeusi lililokuwa na watu wawili, dereva na mtu mwingine.

Baada ya hatua kama 50 hivi, gari lilisimamishwa na anasema waliwaona wanaume wawili wakiwa wamesimama kando ya barabara, kila mmoja akaingia kupitia kila upande na kuwabana Sharon na Oduor hapo katikati na gari likaondoka. Anasema alilazimishwa kuzima simu na baadaye wakafahamishwa kwamba kwa sababu walitaka sana kumuona gavana, walikuwa wanapelekwa kumuona gavana. Wawili hao walikuwa na silaha.

Oduor anasema hayo yalikuwa mazungumzo ya mwisho kabla yake kukabiliana nao na akaruka nje ya gari likiwa bado linasonga katika eneo la Nyangweso, katika barabara ya kutoka Homa Bay kwenda Kisumu.

Baada ya mwendo wa mita kadha, watu wawili – mmoja aliyekuwa ameketi upande wa Oduor na aliyekuwa ameketi mbele pamoja na dereva walitoka na kuanza kumfuata. Aliyekuwa ameketi upande wa Sharon ni kana kwamba hakuondoka kwenye gari.

Oduor anasema alikimbia na kwenda hadi kwenye nyumba moja katika eneo hilo na Nyangweso na kuomba msaada. Mtu mmoja alifika na kumsafirisha Oduor hadi kituo cha polisi cha Adiedo ambapo alimkabidhi kwa polisi. Mwandishi huyo baadaye alisafirishwa kwa gari la polisi hadi kituo cha polisi cha Kendu Bay ambapo aliandikisha taarifa kuhusu yaliyojiri.

Oduor baadaye alichukuliwa na waandishi wenzake wa Nation Media group na kupelekwa hospitali ya Aga Khan, Kisumu kwa matibabu zaidi. Alikuwa ameumia magotini na mikononi.

Anasema alipokuwa anakimbia na kutoroka, hakudhani kwamba wanaume hao wangemdhuru Sharon.

Mwili wa Sharon baadaye ulipatika ukiwa umetupwa vichakani eneo la Oyugis, Homa Bay mnamo 5 Septemba.

Mtaalamu mkuu wa upasuaji wa maiti Kenya Johansen Oduor, baada ya kuuchunguza mwili wa marehemu, alisema mwanamke huyo huenda alifariki kutokana na kuvuja damu sana.

Alikuwa amedungwa kisu mara nane. Mwili huo pia ulikuwa na alama za kukabwa shingoni, na alama nyingine zinazoashiria kwamba alijaribu kujiokoa.

Dkt Oduor alisema kuna uwezekano kwamba Sharon alibakwa.

Wa kwanza kukamatwa alikuwa msaidizi wa gavana Michael Oyamo ambaye baada ya kuzuiliwa kwa muda Homa Bay alihamishiwa Nairobi. Alhamisi, jaji aliwakubalia polisi wamzuilie kwa wiki mbili huku wakiendelea na uchunguzi.

Diwani wa zamani wa wadi ya Kanyidoto Lawrence Mula naye alikamatwa Jumapili 9, Septemba. Kuna washukiwa wengine wanane ambao pia wanazuiliwa na polisi.

Familia imesema mipango ya mazishi ya Sharon kwa sasa imesitishwa hadi ukweli ujulikane
Familia imesema mipango ya mazishi ya Sharon kwa sasa imesitishwa hadi ukweli ujulikane

Familia yake imesitisha kwa muda usiojulikana mipango ya mazishi ya marehemu na Jumatano waliwaambia wanahabari kwamba wanasubiri matokeo ya uchunguzi kuhusu kifo chake.

Wazazi wa Sharon, Douglas Otieno na Melida Auma, wanasema wanataka kwanza kuona waliohusika wakiadhibiwa.

Familia hiyo hata hivyo imeendelea na mpango wa mazishi ya kijusi. Awali, mpango wa kuuzika mwili wa mtoto huyo ulikuwa Alhamisi lakini sasa mazishi hayo yamehamishwa hadi Ijumaa.

Gavana Okoth Obado anayedaiwa kuwa na uhusiano na mwanamke huyo amekanusha kuhusika kwa vyovyote vile na mauaji hayo.

Jumatano, aliitisha kikao na wanahabari Nairobi akisindikizwa na mkewe Hellen Okoth, na wana wao wawili Evaline Okoth na Jerry Okoth.

“Naziomba idara zote za uchunguzi kuharakisha kuhakikisha wauaji wanakamatwa na kuadhibiwa haraka iwezekanavyo,” alisema.

Awali alikuwa ameandikisha taarifa kwa polisi baada ya kuhojiwa kwa saa kadha Kisumu, ambapo taarifa za vyombo vya habari Kenya zinasema alikiri kwamba alikuwa na uhusiano na Sharon.