Mtoto mchanga wa siku moja amenusurika kifo baada ya kuokolewa na mbwa katika kijiji cha Dodo wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba.

Watu walioshuhudia wamesema walimuona mbwa akiwa amembeba mtoto huyo mdomoni mwake ambaye inaaminika alikua ametelekezwa kichakani na Mama yake muda mfupi tu baada ya kuzaliwa.

Wameengeza kuwa kufuatia tukio hilo walitoa taarifa kwa uongozi wa Shehia ya pujini ambapo nawo walichukua hatua ya kuripoti kituo cha polisi cha Chakechake kuhusiana na kadhia hiyo.

Nae Afisa Dawati la jinsia, wanawake na watoto wa jeshi la polisi wilaya ya chakechake Zuwena Hamad Ali amethibitisha kumpokea mtoto huyo kutoka kwa Naibu sheha wa Dodo kibaridi ambae alimfikisha kituoni hapo.

Amesema baada ya kumaliza kumuhoji Naibu Sheha huyo waliwasiliana na Idara ya Ustawi wa Jamii ili kuwakabidhi mtoto huyo kwa lengo la kumfikisha hospitali kwa uchunguzi na matibabu mengine.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Chakechake Omar Mohamed Ali amesema kwa mujibu wa Daktari aliyempokea motto huyo kuwa hali yake inaendelea vizuri.

Aidha amewasihi baadhi ya wanawake wenye tabia ya kuwatelekeza watoto wasiokuwa na hatia kuacha kufanya hivyo kwani ni kosa kisheria.