Leo Agost 9, 2018 ni siku ya uzinduzi rasmi wa sherehe za kutimiza miaka 20 kwa Mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1998.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi mwendeshaji wa mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar ZSSF Ndg. Sabra Issa Machano amesema katika kushangiria miaka 20 ya mfuko wao, ZSSF wameandaa mambo mbalimbali ambayo yanalenga kuwagusa na kuwanufaisha wanachama wake na jamii kwa ujumla.

zssf

Miongoni mwa mambo waliyoandaa ni:

  1. Agosti 13, 2018, majira ya saa 09:00 Alaasiri- ZSSF itafanya Uzinduzi Rasmi wa makumbusho ya mapinduzi yaliopo ndani ya mnara wa mapinduzi ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa habari, utalii na mambo ya kale Mhe. Mahmoud Thabit Kombo.
  2. Agosti 14, 2018, majira ya saa 03:00 Asubuhi – ZSSF itafanya uzinduzi wa jengo la biashara Jumba la Treni “Chawl Building” Darajani ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.
  3. Agosti 15, 2018 majira ya saa 03:00 Asubuhi – ZSSF itakabidhi msaada wa vitanda katika Hospitali ya Mnazimmoja, vitakabidhiwa kwa uongozi wa Wizara ya afya Zanzibar.
  4. Agosti 15, 2018 majira ya saa 08:00 Mchana – Utiaji saini ujenzi wa jengo la biashara Michenzani “Michenzani Shoping Mall” baina ya ZSSF na Kampuni iliyoteuliwa kusimamia ujenzi huo.
  5. Agosti 16, 2018 – ZSSF itafanya Semina ya kujiandaa kustaafu kwa wastaafu watarajiwa itakayofanyika katika ukumbi wa Mikutano Kariakoo Unguja.
  6. Agosti 17, 2018 majira ya saa 09:00 Mchana hadi saa 03:00 Usiku – ZSSF itatoa ofa kwa wanachama wake wote kuingia bure katika viwanja vya kufurahishia watoto vya Kariakoo na Tibirinzi Pemba.
  7. Agosti 20, 2018 ambayo ndio kilele cha sherehe hizo ZSSF itafanya mkutano mkuu wa mwaka na wadau wake kutathmini juu ya mafanikio na changamoto za mfuko wao ambapo mgeni rasmi atakuwa Makamu wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Kauli mbiu ya sherehe za kutimiza miaka 20 ya ZSSF ni “Mafanikio yako Mwanachama ni mafanikio yetu” ( your benefit, our Success).