Wakilishi wa Zanzibar michuano ya Klabu Bingwa Afrika JKU SC wanatarajia kumaliza mchezo wao wa mzunguko wa pili leo kwenye uwanja wa Amani majira ya saa kumi za jioni.

JKU SC watacheza dhidi ya Al Hilali ya Sudan ambapo kwenye mchezo wa awali kule Khatum Sudan JKU walipokea kichapo cha goli 4 kwa bila majibu dhidi ya wababe hao wa Ligi kuu ya Sudan mchezo uliochezwa tarehe 27 mwezi wa 11.

JKU SC wanahitaji magoli matano kwa bila ndipo ijihakikishie kufuzu hatua ya mzunguko mwengine wa tatu ili kufikia hatua ya makundi ya klabu Bingwa Afrika CAF.

JKU SC ikipoteza mchezo huo itakuwa rekodi ya vilabu vya Zanzibar kufanya vibaya inaendelea kuwepo kwenye mashindano hayo ya kimataifa.

Zanzibar24 imezugumza na baadhi ya wadau wa mpira wa miguu Zanzibar wamesema ni kawaida kwa vilabu vya Zanzibar kufanya vibaya kwenye mashindano hayo ya Afrika .

Ali Salum yeye ametaka vilabu vya Zanzibar kubadilika na kuona ipo haja ya kufumua mfumo wa uongozi ndani ya vilabu vya Zanzibar ambavyo kimsingi havifanyi bidii ya kuonyesha kuwa wao ni washindani wa kimataifa Zaidi.