Gavana wa jimbo la Nairobi Mike Sonko ameisimamisha kazi bodi nzima ya usimamizi ya hospitali ya kujifungulia kina mama ya Pumwani mjini Nairobi.

Hii ni baada ya kushtukiwa miili 12 ya watoto wachanga iliopatikana ikiwa imefichwa kwenye maboksi katika hali ya kutatanisha.

Miili hiyo ilikua imefungwa pamoja katika karatasi za plastiki na kuwekwa ndani ya boksi na kuwekwa ndani ya chumba kimoja badala ya miili hiyo kupelekwa katika chumba cha kihifadhia maiti.

Sonko amesema kuwa aliaamua kufanya ziara ya kushutukiza katika hospitali hiyo baada ya kupokea kanda ya video inayoonyesha wafanyikazi wakiindoa miili hiyo kutoka kwenye wodi.

”Nimetembelea ghafla hospitali ya Pumwani kufuatia malalamishi ya umma kwamba usimamizi wa hospitali hii iliamua kuzima umeme katika kitengo cha kinamama kujifungulia, bila maelezo yoyote hatua ambayo ilisababisha vifo vya watoto hawa wachanga”

Tukio hilo limewashutusha wengi nchini Kenya, huku baadhi wakieleza hasira yao kuhusu uamuzi wa wachache walioona kwamba watoto hao wachanga hawastahili kuishi

Hii sio mara ya kwanza kwa hospitali hiyo ya Pumwani kumulikwa katika vyombo vya habari Kenya kutokana na matatizo na kashfa kuhusu akina mama wanaojifungua watoto katika hospitali hiyo na huduma wanazopokea.

Sonko amesema kuwa maisha ya binadamu lazima iheshimiwe na kuongeza kuwa hatua kali itachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakaye patikana na hatia ya kuhujumu huduma nzuri inayotolewa kwa wanawake wanaojifungulia katika hospitali hiyo.

Gavana huyo wa Nairobi pia amemteua Dr Simon Mueke kama afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo ili kuhakikisha shughuli za kila siku zinaendeshwa kama kawaidi huku uchunguzi dhidi ya maafisa walio simamishwa kazi ukiendelea.

Hospitali ya Pumwani ni moja ya vituo vikuu vya kujifungulia kinamama mjini Nairobi,Lakini hospitali hiyo imekumbwa na utata kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na madai ya unyanyasaji dhidi ya wanawake wajawazito, na kuiba na kuuzwa kwa watoto wanaozaliwa katika hospitali hiyo.