Mitawi ataka tafiti zifanyiwe kazi ipasavyo

Mwenyekiti wa Kamati ya taifa ya utafiti Abdallah Hassan Mitawi ambae ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa pili wa Raisi Zanzibar amesema ili kufikia malengo ya serikali ya kukuza uchumi na kuondokana na umaskini ni lazima tafiti zinazozalishwa na watendaji wa taasisi mbalimbali zifanyiwe kazi ipasavyo.

Akizungumza katika kikao cha Wajumbe wa kamati hizo Huko Ofisi za Mtakwimu Mkuu Mazizini amesema tafiti nyingi zinazofanywa zimelengwa kusaidia kuleta maendeleo  kwani nchi nyingi zinazoendelea dunia zimekuwa zikizifanyia kazi tafiti zinazozalishwa na wataalamu.

Amesema Tafiti zikifanyika husaidia kwenye maeneo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi ikiwemo kwenye Kilimo,Uvuvi,Biashara,Afya na hata elimu hivyo  watendaji wanapaswa kuajibika ili kufanikisha malengo ya serikali katika kuondokana na umaskini na hali duni za kimaisha.

Hata hivyo Mitawi amesema changamoto kubwa inayojitokeza kwenye fatiti zinazofanywa nchini ni kutofanyiwa kazi na kuishia ndani ya makabati hivyo uwazishwaji wa mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa tafiti hizo utasaidia kufanyiwa kazi kwa haraka.

Kwaupande wake Katibu  Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Khalid Bakari Hamrani amesema  kamati itaendelea  kusimamia tafiti zinazozalishwa hasa za watafiti wa nje wanaokuja kuomba vibali kwaajili ya kufanya utafiti kwamba hawakiuki masharti wanayopangiwa ili kuepusha udanganyifu  ambao utaweza kuleta matatizo kwenye  nchi.

Kikao hicho kilichowashirikisha watendaji mbalimbali kutoka taasisi za serikali ambapo jumla ya tafiti mia moja na saba zilifanywa kuanzia  Juni hadi oktoba  zilizoshirikisha watafiti wageni na wenyeji  zilizohusisha masula ya kilimo,mazingira,ustawi wa jamii na historia.