Mjini Magharibi wapata wawakilishi wa mpira wa kikapu Elimu bila Malipo

Mkoa wa Mjini Magharibi umepata wawakilishi wake wa mchezo wa Mpira wa Kikapu watakaowakilisha Mkoa huo kwenye Mashindano ya Michezo ya Elimu Bila ya Malipo ngazi ya Taifa yatakayoanza Septemba 18 hadi 23 mwaka huu ambapo kilele chake kitafanyika katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.

 

Timu zilizopata nafasi kwenda kwenye Mashindano ya Taifa ya Elimu Bila ya Malipo kutoka Mkoa huo kwa upande wa Sekondari ni Skuli ya Haile Salas Wanaume na Regeza Mwendo Wanawake ambapo kwa Msingi ni Skuli ya Kijichi kwa Wanaume na Shauri Moyo kwa Wanawake.

 

Akikabidhi zawadi kwa Washindi hao Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud kwenye Michezo ya mwisho iliyochezwa kwenye Uwanja wa Maisara asubuhi ya leo, Mkuu huyo amewataka Walimu kujua wajibu wao wa kuhakikisha Wanafunzi wanapatiwa haki yao ya kushiriki Michezo.

 

Amesema Michezo ni sehemu muhimu kwenye Elimu huku akiwapa hamasa timu hizo kuwaandalia zawadi nono watakapochukua Ubingwa kwenye Mashindano ya Elimu Bila ya Malipo ya Taifa kwa kuuwakilisha vyema Mkoa huo.

Aidha amezitaka timu hizo kuwakilisha vyema kwenye mashindano na kuwahidi kila timu ya mkoa wa mjini Magharibi itakayoshinda itapatiwa kiasi cha Tsh 100, 00 laki moja na walimu wao wa michezo.

 

‘’Nawaomba walimu na wazazi wahakikishe wanawalinda watoto hawa na udhalilishaji ili kulinda vipaji vyao vya baadae tutahakikiSha tunapambana na udhalilishaji’’ Alimalizia mkuu wa Mkoa Ayubu Muhamed.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Michezo na Utamaduni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amaali Zanzibar Hassan Hairal Tawakal amesema mafanikio na hamasa ya Mashindano hayo ni matunda ya kuwepo mpango wa sports 55 ambao umebuniwa Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Mohamed Ali  Shein.

 

Aidha amesema mpango wa Sports 55 umekuja kukomboa michezo maskulini kwa kuja na mpango wa kuzindua vipaji mashuleni na kurejesha hamasa ya michezo maskulini.

 

‘’Tuta jitahidi sana kuhakikisha tunakuwa na mashindano yaliyo bora na yenye mvuto kwenye tamasha la mwaka huu na zawadi bora na nzuri kwa washindi wote ‘’ Alisema Tawakal.