RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Bejamin William Mkapa aliyahifadhi na kuyalida Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa vitendo.

Pia, Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Marehemu mzee Mkapa aliuhifadhi na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo hivyo, ataendelea kuheshimiwa kwa ari yake hiyo na uzalendo wake huo aliokuwa nao.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo wakati akitoa salamu za wananchi wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia kifo cha Marehemu Rais Bejamin William Mkapa katika maziko yaliyofanyika huko kijijini kwake Lupaso, Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Masasi.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa wananchi wataendelea kumuenzi na kumkumbuka Rais Mkapa katika maisha yao yote sambamba na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu.

“Takribani siku hizi sita zilizopita tulikuwa na majonzi makubwa lakini hatukusikitika kwani ndio uwezo wa Mwenyezi Mungu, hivyo ni jukumu letu kumuombea Mzee wetu huyu ili MwenyeziMungu amsamehe makosa yake na amjaalie amuweke mahala pema”

“Mwenyezi Mungu atupe hatima njema ya maisha yetu hapa duniani tukitimiza wajibu wetu katika kutekeleza majukumu yetu kama vile alivyofanya kiongozi wetu huyu Rais Benjamin William Mkapa”, alisema Rais Dk. Shein.

Hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa majonzi makubwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wote  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  wananchi wa Mkoa wa Mtwara na hasa Wilaya hiyo ya Masasi katika maombolezo ya msiba huo mkubwa.

Aidha, Rais Dk. Shein alimtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kupokea salamu hizo za wananchi wa Zanzibar huku akisisitza kwamba safari hiyo ya umauti ni ya mwisho ambayo ni muhimu na ya  lazima kwa kila mwanaadamu.