Mkutano wa kimataifa wa viongozi wa dini ya Kiislamu na Kikiristo wafanyika Zanzibar

Shirika la roho Mtakatifu limesema litaendelea kushirikiana na viongozi wa dini mbalimbali  ili kuimarisha amani na utulivu  iliyopo nchini pamoja na kushirikiana katika shughuli za maendeleo kwenye jamii.

Akizungumza na Waandishi wa habari Baada ya mkutano wa kimataifa wenye lengo la kujenga amani na udugu baina ya Waumini wa dini ya kikiristo na Waislamu uliofanyika Welezo Mjini Zanzibar , Father Florentine Mallya amesema ni vyema  kwa Viongozi wa dini ya kikiristo na dini ya kiislamu kuendelea kushirikiana  katika kuhubiri amani iliyopo.

Amesema Viongozi wa dini kutoka Nchi mbali mbali wamekuwa wakija Tanzania Bara na Visiwani kujifunzi jinsi Watanzania wanavyotunza amani hivyo si vyema kujishirikisha katika masuala ya uvunjifu wa amani yanayosababishwa na tofauti za kidini.

Kwa upande wake Katibu wa Mufti Zanzibar Shekh Fadhil Suleiman Soraga  Pamoja na Askofu Dk.Alex Malasusa kutoka kanisa la KKKT Dar es salam wamesema  Watahakikisha wanashirikiana pamoja katika kusaidia jamii inayowazunguka pamoja na kuhubiri amani katika mihadhara ya dini.

Wamesema wafuasi wa dini zote mbili hawaweze kuendelea na ibada zao kama hapatakuwepo amani na usalama wa Nchi hivyo wataendelea kusimamia suala hilo kwa lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika kuimarisha amani ili kuimarisha shughuli za maendeleo hususan katika sekta ya utalii.

Mkutano huo wa Kwanza wa kimataifa wa  wiki moja wenye lengo la kujenga amani na udugu baina ya Waumini wa dini ya kikiristo na Waislamu,umeshirikisha viongozi wa nchi 16 ikiwemo Tanzania, Ulaya na Marekani pia unaendelea kufanyika hapa Zanzibar.