Hukumu ya anayetajwa kuwa mlanguzi mkubwa wa dawa za kulevya Baktash Akasha inatarajiwa kutolewa baadae leo mjini New York nchini Marekani.

Baktash na nduguyake Ibrahim walikamatwa mjini Mombasa mwaka 2014 wakiwa pamoja na raia kutoka Pakistani na mwingine wa India.

Ndugu hao wa Akasha wanatuhumiwa kutumia ghasia, mauaji na kutoa hongo kulinda biashara yao. Wanatuhumiwa kupanga mauaji ya mhalifu raia wa Afrika Kusini anayefahamika kwa jina moja pekee ‘Pinky’.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, Hukumu hiyo inatarajiwa leo wakati taarifa zinaeleza kuwa afisa wa zamani katika idara ya upelelezi nchini DCI, majaji kadhaa na maafisa wengine wa serikali huenda wakahamishwa kupelekwa Marekani kukabiliwa na mashtaka yanayohusu ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Gazeti la Nation nchini Kenya linaripoti kuwa duru zinaarifu kwamba serikali ya Marekani tayari imeifahamisha kuhusu nia hiyo ya kuwashtaki washukiwa katika mahakama za Marekani.

Hatua inayomaanisha kwamba huenda katika siku zijazo kukashuhudiwa kuwasilishwa kwa washukiwa kwa maafisa wa usalama Marekani.