Morocco kuja na sheria mpya itakayowalinda wanawake na unyanyasaji wa kingono

Sheria mpya ambayo inafanya unyanyasaji wa kingono na Udhalilishaji kuwa ni Uhalifu itaanza kutekelezwa nchini Morocco hivi karibuni.

Picha hii ni ya mwanamke aliyebakwa na kulazimishwa kuchorwa michoro mwilini na wabakaji

Sheria hiyo ambayo inajumuisha upigaji marufuku wa ndoa za kulazimishwa, inafuatia kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika miaka ya hivi karibuni juu ya kiwango cha udhalilishaji wanawake.

Utafiti mmoja uliofanywa nchini humo, umeonesha kuwa wanawake sita kati ya 10 nchini Morocco wamepitia manyanyaso hayo.

Matukio ya ubakaji ya hivi karibuni yametangazwa sana katika mitandao ya kijamiii.

Mwandishi wa BBC mjini Rabat amesema sheria hiyo mpya imepokelewa vizuri lakini pia imekosolewa kwa sababu haitoi maana kamili ya unyanyasaji majumbani au marufuku katika vitendo vya ubakaji ndani ya ndoa.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wale wote watakaotiwa hatiani kwa makosa ya kudhalilisha kingono hadharani iwe kwa kutumia maneno, ama ishara yoyote ya kudhalilisha kijinsia atakabiliwa na hukumu ya kifungo kuanzia mwezi mmoja mpaka sita gerezani na pia faini ya fedha taslimu.

Mashirika ya haki za binadamu yanasema kuwa wanawake wengi nchini Morocco wamekuwa ni wahanga wa matukio ya unyanyasaji kingono.

Katika ripoti yake ya mwaka 2015, Shirika la Haki za Binadamu nchini humo limearifu kuwa zaidi ya asilimia 20 ya wanawake nchini Morocco wamekumbwa na matukio ya unyanyasaji wa kingono japo mara moja katika maisha yao

Katika siku za hivi karibuni polisi nchini humo iliwakamata vijana 12 kwa tuhuma za kumbaka msichana wa miaka 17 na kumtesa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.