Mradi wa PAZA umenipa ujasiri- Sichana


Sichana Othman Suleiman

Mjumbe wa Jumuiya ya Vijana ya kupambana na udhalilishaji Mkoa wa Kaskazini Unguja, Sichana Othman Suleiman (28) amesema amekuwa jasiri baada ya kupata elimu ya kujiamini kupitia Mradi wa Kukuza Uwajibikaji Zanzibar (PAZA) na sasa amekuwa mbunifu wa miradi mbali mbali.

Kauli hiyo imetolewa katika mahojiano maalumu ya Mwandishi wa habari hizi wa Zanzibar24 blog wakati akitembelea maeneo yenye mradi wa kukuza uwajibikaji Zanzibar PAZA unaotekelezwa  na taasisi tatu ikiwemo Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Zanzibar, Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) na Jumuiya ya Uhifadhi wa Msitu wa Ngezi Pemba (NGENARECO).

Sichana alisema Mradi huo wa PAZA umemsaidia kuibua njia mbadala za kujitafutia pesa kwa ajili ya maisha yake ambazo zimeweza kumuonesha njia sahihi za kubuni miradi tofauti pasi na malipo yeyote katika mradi huo.

Amesema mradi huo umemjengea uwezo mkubwa wa kujiamini sehemu yeyote ambayo imezungukwa na mkusanyiko wa watu bila ya wasiwasi wowote.

Sichana ni Mkaazi wa Nnjooni Mto wa Pwani Wilaya ya Kaskazini A Unguja amesimulia kuwa mradi wa uwajibikaji Zanzibar umemuwezesha kujua miradi mbali mbali pamoja na kuielimisha jamii kwa kuwapa mafunzo aliyoyapata katika mradi huo ikiwemo Ushoni, Ufumaji na hata kilimo.

’’Naitumia hii elimu yangu nilioipata katika mradi wa PAZA kwa kuwaelimisha wenzangu waliokuwa hawajishuulishi na kitu chochote wapo wamo tu na nashukuru  wamenifahamu na pia wamenikubali  na sasa mafunzo niliyowapa wanayafanyia kazi na tayari faida yake tunaiona”

Amesema yeye pamoja na wenzake ambao wamepata mafanikio wanajivunia kwa kuwa wameweza kujikwamua kiuchumi kwa kiasi fulani.

“Sasa mimi pamoja na wenzangu tumefanikiwa kupata eneo tulilootesha mimea ya ‘sun flour’ na sasa najipatia pesa kutokana na biashara zangu za ufumaji wa mikoba maana sasa hadi tenda najipatia’ ’Aliongeza Sichana.

Akielezea kujiunga kwake na jumuiya ya Vijana ya kupambana na udhalilishaji alisema.

’’Nimeamua kujiunga na Jumuiya ya Vijana kupambana na udhalilishaji kwasababu ya kupata uzoefu wa utendaji kazi katika jamii, pia kuunda timu pamoja na vijana wenzangu ili kupatikana kwa fursa nzuri ya utoaji elimu na kupelekea jamii kuondokanana vitendo vya udhalilishaji na hata kuibua biashara tofauti kwa kujiondolea hali duni ya maisha yaani kuondokana na utegemezi’’

Akitoa ushauri kwa jamii amesema kuwa jamii ijijengee tabia ya kubuni miradi tofauti kwa lengo la kuwasaidia kimaisha pasipo na kukaa bure kusubiri kuajiriwa Serikalini

Sichana Othman Suleiman ambae kwa sasa ana elimu ya Diploma katika chuo cha Dar-es-salaam Collage of Hotel and bussiness  Students kilichopo Vuga nyuma ya Mahkama kuu Zanzibar pia amesomea ujasiri amali katika taasisi ya iliopo Mwanakwereke ndani ya Jengo la Chuo cha mafunzo ya amali Zanzibar.

Mradi wa Kukuza Uwajibikaji, Promote Accountability Zanzibar (PAZA) unafanya kazi katika shehia za Unguja na Pemba kwa kushirikiana na Asasi za kiraia, Halmashauri na wana mitandao na unasimamiwa na ZANSAP na kufadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya, European Union (EU)