Mwanamuziki na Muandaaji wa muziki nchini Marekani, Pharrell Williams amemlima barua Rais wa Taifa hilo, Donald Trump inayomtaka asitumie tena wimbo wake wa ‘HAPPY’ kwenye shughuli zake za kisiasa.

Pharrell amechukua maamuzi hayo, baada ya Rais Trump kuutumia wimbo huo Wikiendi iliyopita katika Mkutano wake wa Kisiasa mjini Pittsburgh katika eneo ambalo masaa machache yaliyopita kabla ya mkutano huo, kulitokea mauaji ya watu 11 katika Sinagogi la Wayahudi.

Siku hiyo hiyo ndani ya eneo moja, watu 11 wameuawa halafu masaa machache unacheza wimbo wa Happy inaingia akilini? tena kwenye masuala ya kisiasa. Sisi kama wanasheria tumeafikiana na Mteja wetu kuwa Rais huyo asiutumie tena wimbo huo na akirudia kufanya hivyo tutampeleka mahakamani kwa makosa ya Copyrights na ‘trademark rights’,“ameeleza Mwanasheria wa Pharrell Williams aliyejitambulisha kwa jina la Howard King.

Mwanasheria huyo amedai kuwa kitendo cha Trump kucheza wimbo huo jukwaani, ni kitendo cha kichochezi na kina weza tafsiriwa vibaya kwa wananchi wa eneo la Pittsburgh huko Indiana.

Kwa muda mrefu Pharrell (45) amekuwa akikipigia upatu chama cha Democratic, ambacho ndio chama pinzani kikubwa nchini Marekani dhidi ya Chama tawala cha Republican cha Donald Trump.