Mtangazaji na Muandishi wa Michezo wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Abubakar Khatib (Kisandu) ameshinda nafasi ya Makamo Mwenyekiti kwenye Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kusini Unguja (SOURFA) uchaguzi uliofanyika Dunga Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi Silima Hassan Omar amesema Kisandu amemshinda Jina Suleiman Hassan kwa kura 10-9 Uchaguzi ambao ulikuwa na upinzani mkubwa kutokana kujitokeza  Wagombea wengi kuwania nafasi za uongozi kwenye Chama hicho, huku akiwataka washindi hao kuyatekeleza yale yote waliyoyaahidi kwenye kampeni zao.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi hao wapya Kisandu amesisitiza Mashirikiano kwa wadau wote wa soka wa mkoa huo kwa lengo la kujenga Kusini mpya ya soka.

Wengine waloshinda kwenye uchaguzi huo ni Shauri Hassan Jaku aliyemmwaga Ussi Jecha Haji kwa kura 10-9 ambapo Masoud Ali Dau amefanikiwa kushinda nafasi ya Ukatibu kwa kumshinda Mussa Kinole Mussa kwa kura 10-8 wakati Mohd Idrissa Haji ameshinda nafasi ya katibu msaidizi kwa kupata kura 10-9 dhidi ya Hassan Ali Mohd.

Mwana mama Zul-Khudhaifa Suleiman Hassan ameshinda nafasi ya Mshika fedha na kusaidiwa na Safi Miraji Abdallah aliyeshinda nafasi ya Mshika Fedha msaidizi.

Wajumbe wa kamati Tendaji waliochaguliwa ni Shaabani Naimu Suleiman (Kura 13), Sabahi Baraka Hassan (Kura 11) na Haji Khatib Ali (Kura 11) huku Muazini Jogoo ameshinda nafasi ya Muwakilishi wa Vilabu kutoka Wilaya ya Kusini na Seif Ali Ameir amechaguliwa kuwa Muwakilishi wa Vilabu kutoka Wilaya ya Kati.