Mtoto mwenye umri wa miaka 10, jina (limehifadhiwa) ameisimulia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jinsi alivyoshuhudia  baba yao wa kambo, Godfrey Samweli au Nkwabi akimnyonga mama yake Bahati Hussein na kimsababishia kifo.

Mtoto huyo anayesoma darasa la tatu, leo Julai 3/2019 ameeleza mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu, Pamela Mazengo kuwa alishtuka usingizini wakati wa usiku na kumshuhudia baba yao akimkunja shingo mama yake kama anaivunja na kumwambia asipige kelele.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Erick Shija, kutoa ushahidi  wake dhidi ya kesi ya mauaji inayomkabili Godfrey, mtoto huyo ambae ni shahidi wa tatu kati ya mashahidi watano waliotoa ushahidi leo, amedai mama yake amefariki mwaka 2014.

Akitumia takribani dakika tano kuelezea alichoona, mtoto huyo amedai kuwa, Juni 20,2014 yeye ambae wakati huo alikuwa na miaka mitano akiwa amdogo wake Rahimu ambao walikuwa wanalala chumba kimoja na wazazi wao hao ambapo baba na mama yao wanalala kitandani huku wao wakilala chini kwenye godoro walienda kulala kati ya saa 2 au 3 usiku lakini baadaye usiku alishituka na kuona mama yake akirusha rusha miguu na kumwambia asipige kelele ndipo alipomnyonga mama yao.

Amedai kuwa, alinyamaza hakupiga kelele, baadae usingizi  ulimpitia hadi asubuhi ambapo alipoamka alimuona mama yake akiwa amelala kitandani na hakujua kama alikuwa amekufa, 
alifungua mlango wa chumbani ambao haikuwa imefungwa na kutoka nje ambapo alienda kupiga mswaki na kwenda kucheza. Lakini akiwa anacheza alisikia kelele nyumbani kwao na alipofika ndugu zake walimwambia kuwa mama yao amefariki.

Ameongeza kwamba siku hiyo hakumuona baba yake (Godfrey) kuanzia alipoamka

Ameeleza kuwa, kwa marehemu mama yake wamezaliwa watoto wanne ambao ni Hadija, Hassan, Hemed na yeye mwenyewe na kwa baba huyo hakuwa na mtoto na mama yao.

Naye mtoto wa pili wa marehemu, Hadija Juma (16) ambae wakati mama yake anauwawa alikuwa na miaka 10 amedai, Juni 20,2014 alienda kulala kati ya saa 5 au 6 usiku akiwa na mtoto wa mama yake mdogo anayeitwa Mwanahamisi Hussein ambapo usiku mkubwa alisikia mama na baba yake wanagombana na kumpelekea, mdogo wake kuogopa  lakini alimtoa hofu nakumwambia asiogope kwani wanaongea kuhusu ugomvi wao wa mchana.

“Hata hivyo, hatukulala tulikaa kitandani na mdogo wangu akaniambia nimpeleke kukojoa  tukatoka na tulipofunua pazia tulimuona Godfrey akiwa amekaa kwenye kochi huku amevaa kipensi na shati liko begani huku akitokwa na jasho,” amedai na kuongeza; walipofika hapo sebuleni, Godfrey alituuliza tunaenda wapi mimi nikamwambia tunaenda kukojoa akatujibu sawa…, tulienda kukojoa na kurudi chumbani…baadaye nilimsikia akifungua mlango wa sebuleni na kutoka nje alipotoka tulijificha nyuma ya mlango wa sebuleni,” alidai.

Akiendelea kitoa ushahidi wake, shahidi huyo  wa pili amedai, walimsikia baba yao akigonga mlango wa chumba cha jirani na kumuuliza kama amesikia chochote lakini walisikia yule kijana akimjibu kuwa hajasikia chochote na kumwambia akalale

Shahidi huyo alipoulizwa alijuaje kama aliyekuwa akigonga kwa jirani ni Godfrey alidai kuwa, anaitambua sauti ya baba yake huyo.

Ameendelea kudai kuwa, walisubiri kuona kama baba yao kama angeingia ndani lakini hawakusikia chochote mpaka wakapotiwa na usingizi hadi asubuhi alipoamshwa na mama mwenye nyumba akimtaka apeleke vyombo chumbani kwa mama yake.

Akadai, aligonga chumbani kwa mama yake zaidi ya mara moja lakini hakufungua na alipofungua mlango alimuona mama yake akiwa amefunikwa shuka jeupe na alipomfunua aliona kipande cha kanga mdomoni, alama za kucha shingoni na alianza kumtingisha huku akimuita lakini hakuitika na mapigo ya moyo yakiwa yamesimama.


Amedai alipiga kelele huku akikimbilia nje ndipo mama mwenye nyumba alimuuliza kuna nini na alipomwambia alikataa kuingia ndani na kwenda kumuita mama yake mdogo ambaye nae aliogopa kuingia ndani humo mpaka majirani walipofika pamoja na dada yake Hadija Shaban ambao waliingia ndani na kumuhifadhi mama yao kisha wakampeleka polisi na baadae hosp. Ambapo alipewa taarifa ya kifo baadae baada ya ndugu zake kutoka hospitali ya Amana.

“Kabla mama hajafariki aliwahi kuniambia kwamba akifa atakayemuua ni Godfrey. Lakini kuna kipindi niliwahi kumsikia mara mbili akimwambia mama kwamba atamuua na familia yetu popote itakapoiona ataiua. Pia kuliwahi kuwa na ugomvi kati ya mama na Godfrey akitaka kuuza nyumba tuliokuwa tumepanga na mama alimkataza,” alidai Hadija.

Naye, sahidi wa kwanza katika kesi hiyo ya mauaji, Hadija Shabani (26)  amedai Juni 20, 2014 alienda kwa shangazi yake Bahati na kumkuta na ugomvi baada ya Godfrey kumuhisi mkewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi na jirani yake.

Shabani alidai baada ya marumbano ya muda mrefu alifika Mrisho Hussein ambaye ni mdogo wa shangazi yao na kusuluhisha ugomvi huo na yeye aliondoka Ulongoni saa 2 usiku kwenda nyumbani kwake Vingunguti.

Alidai saa 11 alfajiri alipigiwa simu na Godfrey akimtaka aongee na shangazi yake akamwambia hawezi kwenda nyumbani muda huo asubiri hadi asubuhi na alipofika nyumbani kwa Bahati walimkuta akiwa amefunikwa na alama za kucha shingoni na walimpeleka hospitali na kugundulika amekufa.

Mama mwenye nyumba waliyopanga Godfrey na Bahati, Fatuma Adam (46) alidai hakusikia ugomvi usiku wa tukio na siku iliyofuata alisikia mtoto wa marehemu akipiga kelele na kwenda kumuita  mdogo wa marehemu  na walisaidia kumuhifadhi marehemu.

Alidai walipomkagua marehemu walimuona na alama za kucha shingoni na kwamba walipompeleka hospitali waliambiwa amefariki.

Hata hivyo, shahidi wa tano alitoa ushahidi wake kuhusu tukio hilo na mahakama iliahirisha kesi hadi Julai 9, mwaka huu kwa kusikilizwa.

Katika kesi hiyo inadaiwai Juni 21, 2014 huko Ulongoni A wilayani Ilala, Dar es Salaam, Godfrey alimuua kwa makusudi mke wake Bahati Hussein.