MAMA mmoja chini Kenya amekatwa mikono yote miwili na mumewe kwa kutumia kisu akidai kwamba ameshindwa  kumzalia watoto, katika kile kinachosemekana ni tukio  baya zaidi la  ugomvi wa nyumbani.

Mama huyo ambaye ni Jackline Mwende  mkaazi wa kijiji cha Kathama , Kaunti ya Machakos  amedumu katika ndoa na mume wake huyo  kwa miaka saba.

Mikono yake  ilikatwa kutoka katika kifundo cha mkono na mumewe Stephen Ngila Thenge  na pia ana majeraha  kichwani  na shingoni  kutokana na shambulio hilo Julai 24 mwaka huu.

Ndugu zake wamesema kuwa wanandoa hao walikuwa na matatizo na kwamba bi Mwende alitaka kumwacha mumewe,lakini akashauriwa kutofanya hivyo na kiongozi mmoja wa dini.

Mwende amesema  kabla ya shambulio hilo,  walikuwa wakiishi mbalimbali na mumewe kwa takriban miezi mitatu kwa kosa la kutopata watoto.

”Sijui kwa nini aikuwa akinilaumu licha ya sisi sote kwenda hospitalini mwaka uliopita na kwamba daktari alisema kuwa ni yeye aliyekuwa na tatizo la kuzaa ambalo linaweza kurekebishwa”.

Amesema kuwa mumewe ambaye ni mshonaji nguo katika mji wa Masii,  alikataa kufuatilia matibabu.