Mume, Mke waokotwa wakiwa wameshafariki porini

Maiti za mume na mke  zimeokotwa katika pori la kijiji cha Gwata Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Mwili wa mwanamke umekutwa na jeraha la kukatwa na kitu kama panga huku mwili wa mwaume ukikutwa ukiwa unaning’inia mfano wa mtu aliyenyongwa.

Akizungumza leo Ijumaa Oktoba 12, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amewataja marehemu kuwa ni Theresia Omary (30) na Jokenis Yohana (35) wakazi wa kijiji cha Gwata, kwamba ni mme na mke.

“Ni kweli tulipokea taarifa kwa raia wema juu ya kuonekana miili ya watu wawili na baada ya askari kufika eneo la tukio jioni jana tulikuta mwanamke ameuawa kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili,” amesema Nyigesa.

“Na mwanaume inadhaniwa ndiye aliyemuua mkewe na kisha na yeye kujinyonga hapo eneo la tukio ila tunachunguza.”

Amesema katika mahojiano waliyofanya na watoto wa marehemu pamoja na majirani wamesema wawili hao juzi jioni waliaga wanakwenda porini kuchimba dawa za kienyeji na hawakurejea hadi miili yao ilipogundulika.

Amesema marehemu wameacha watoto wanne huku akibainisha kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.