Kijana mmoja anaetambulika kwa jina moja la Sadiki, ambaye ni muuza mishikaki katika eneo lililo karibu na jengo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar esalam ashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kukutwa akiuza mishkaki ya paka.

Walaji wengi wa mishkaki ya Sadiki wamekuwa wakipatwa na shaka na nyama hiyo kutokana na ladha yake kuwa tofauti, lakini kila mara wakiuliza kuhusu jambo hilo, jamaa huyo amekuwa akiwatoa wasiwasi kwa kuwaambia kuwa kitoweo hicho ni cha ng’ombe.

Imedaiwa kutokana na shaka ya wateja wa mishkaki hiyo inayoletwa na ladha isiyo ya kawaida ya nyama, ambayo pia hunogeshwa kwa viungo vya aina mbalimbali, wananchi wa eneo hilo waliamua kumuwekea mtego ili kubaini ukweli.

Alhamisi iliyopita, wakati akiwasili katika kijiwe chake kuendelea na kazi yake ya kuuza mishikaki, ghafla wananchi walimvamia na kumnyang’anya ndoo yake ya nyama na kuifungua, ndipo zilipokutwa nyama hizo zilizodaiwa kuwa za paka.

Wananchi wenye jazba baada ya kuona hivyo walitaka kumuangushia kipigo, lakini walitokea polisi wa doria ambao walimuokoa mfanyabiashara huyo na kwenda naye kituoni kumhoji zaidi kuhusiana na tuhuma hizo.