HD1

Wajumbe Kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar- ZEC wanaokiwakilisha chama cha wananchi CUF wamedai kuwa M/kiti wa Tume hiyo Jecha Salim Jesha amepoteza sifa kisheria na kikatiba kusimamia tena uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Visiwani Zanzibar Machi 20 mwaka huu baada ya ule wa Octoba 25 kufutwa kwa madai kutokea dosari kadhaa.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wajumbe hao Ayoub Bakari Hamad pamoja na Nassor Khamis Mohamed wamedai kuwa maamuzi na hatua ya kufuta Uchaguzi halali uliofanyika Octoba 25 visiwani humo kama uliofanywa na Bwana Jecha haukutokana na maridhiano ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar na wajumbe wake.

Aidha wajumbe hao wamesisitiza msimamo wa CUF kutoshiriki Uchaguzi wa Zanzibar wa maruduio ambapo wametaka kuwepo kwa mazungumzo ya kutafuta muafaka kwa maridhiano juu ya sintofahamu kuhusu suala la Zanzibar huku wakitoa angalizo la kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC tayari imetangaza kufanyika kwa Uchaguzi wa marudio kwa Upande wa madiwani,wawakilishi na rais wa zanzibar kwa maelezo kwamba uchaguzi wa octoba 25 ulifutwa na mamlaka halali Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kufuatia kujiridhisha na dosari zilizojitokeza kwenye uchaguzi huo.