Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo – Dkt Harrison Mwakyembe amesema michezo yote iliyosalia ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho itachezwa jijini Dar es Salaam.

Waziri Mwakyembe amesema kufuatia tamko la Rais Dkt. John Magufuli kuruhusu shughuli za michezo kuanza tena Juni Mosi, imetengwa mikoa miwili itakayotumika kama vituo vya mchezo wa soka, kikiwemo kituo cha Dar es Salaam.

Kituo kingine ni mkoa wa Mwanza ambako itachezwa michezo ya Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.

Kwa upande wa viwanja vitakavyotumika, Dkt. Mwakyembe amesema kwa Dar es Salaam utatumika uwanja wa taifa pamoja na viwanja vya Uhuru na Chamazi Complex.

Viwanja vya Mwanza vitakavyotumika ni CCM Kirumba na Nyamagana.