MATUKIO ya watu kuuawa na mamba katika Mto Mkomba, yameendelea kushika kasi huku viongozi wa wilaya ya Nkasi wakiumiza vichwa kutafuta namna ya kudhibiti.

Hali hiyo imetokea baada ya mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kalila kata ya Kabwe wilayani hapo, Laeh Alfonce (5) kupoteza maisha kwa kuliwa na mamba katika mto huo.

Tukio hilo la aina yake lililozua gumzo na taharuki kwa wakazi wa kijiji hicho, limetokea baada ya wazazi wa mtoto huyo walipotoka shambani kwenda katika mto huo kwa ajili ya kuosha vyombo wakiambatana na mtoto huyo. Baada ya kuosha vyombo, ghafla mamba alimkamata mtoto akiwa pembezoni mwa mto huo.

Akisimulia mkasa huo, Diwani wa kata hiyo, Asante Edward, alisema mtoto huyo aliliwa na mamba akiwa na wazazi wake kando kando ya maji ya mto huo na bila kutarajia mamba mkubwa aliibuka na kumvuta mtoto hadi kwenye kina kirefu.

Diwani Edward alisema baada ya mtoto huyo kukamatwa, vilisikika vilio na sauti kubwa za wazazi na watu wengine waliokuwa wakifua nguo wakiomba msaada na ndipo watu wengi wakiwamo viongozi wa kijiji na kata walifika na kutoa msaada.

Alisema baada ya kufika kwenye mto huo, walitoa msaada wa kumsaka mamba huyo, lakini walikuta mtoto tayari amefariki huku baadhi ya viungo vikiwa vimeliwa, hali iliyozua taharuki kubwa kwa wakazi wa kijiji na kata hiyo.

Diwani huyo alisema tukio hilo la mtoto kuliwa na mamba ni la nne kwa mwaka huu. Alisema hali hiyo inatokana na mamba wala watu kuwa wengi kupita kiasi, hivyo aliiomba serikali kuwavuna mamba hao ili kubaki wachache watakaopunguza madhara kwa binadamu.

“Nawaomba wananchi muwe makini wakati mkichota maji au kufua nguo kwani mto huu una mamba wengi na wakali. Kwa sasa nitalipeleka suala hili kwa mkurugenzi mtendaji na hata kujadiliwa kwenye vikao ili mamba hawa wavunwe kulinda usalama wa watu,” alisema.

Alfonce Alfonce, baba wa mtoto huyo, licha ya kujawa na huzuni kutokana na mtoto wake kuuawa na mamba, alikosa nguvu kulizungumzia sakata hilo na muda wote alikuwa akilia.