Wanafunzi wameshauriwa kutochagua masomo wakati wa kipindi cha masomo yao kwa ili kujihakikishia ufaulu wa juu katika mitihani yao ya Taifa .

Akizungumza na Zanzibar24 mwanafunzi bora Tanzania  wa somo la Kiarabu kutoka Skuli ya Al Ihsan Girls Secondary School iliyopo mwanakwerekwe Mkoa wa Mjini Magharib Unguja  Maryam Hassan Ali amesema mafanikio yake yalitokana na jitihada kubwa alikuwa akionyesha akiwa darasani na kushirikiana na wenzake darasani.

Aidha Maryam amesema hakuwa mwanafunzi mwenye kukata tamaa darasani, alikuwa miongoni mwa wanafunzi walikuwa hawasikilizi maneno ya watu wanaobeza masomo ya Sanaa (Arts) kwa kuwa ilikuwa ikiyapa kipaumbele.

Kwa Upande mwengine Maryam amewataka wanafunzi wenziwe wasikate tamaa kwa kuwa masomo ya sanaa (Arts) miongoni mwa masomo yanaweza kukufanya na kukupa nafasi kubwa kwenye jamii hivyo hakuna haja ya kubezwa masomo hayo na pia ni magumu.

“Changamoto zilikuwa nyingi watu walikuwa wakibeza wakinambia Arabic halina mpango halishughulikiwi na halina soko lakini mi sikujali maneno ya watu na leo nimepata ufaulu wa juu kidato cha sita” Alisema Maryam.

Aidha maryam amefunguka na kusema kwa sasa mipango yake ni kujiunga na chuo cha Sumait ngazi ya Shahada ya elimu ya Lugha na ndoto zake siku moja kuwa mwalimu wa masomo ya Lugha.

Kuhusu suala la mikopo Maryam amesema kwa Upande wa familia yake haina uwezo wa kumsomesha chuo kikuu na tayari ameshaomba mkopo wa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na anasubiri udhamini kutoka Shirika la Direct Aid ambao ndio wamiliki wa skuli hiyo ya Al Ihsan Girls Secondary School.

Maryam Hassan amepata ufaulu wa daraja la pili point kumi na moja na amefanikiwa kupata alama B ya somo la Kiarabu katika matokeo yake ya kidato cha sita na kuchukua nafasi ya mwanafunzi bora Tanzania wa somo la kiarabu.