Mwandishi wa habari mashuhuri kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji

Mwandishi wa habari wa runinga ya Citizen ya Kenya Jackie Maribe na mchumba wake Joseph Irungu sasa watapandishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.

Wawili hao wamekuwa kizuizini toka mwezi uliopita kupisha polisi kufanya uchunguzi wa kifo cha mfanyabiashara Monica Kimani, aliyeuawa kwa kukatwa shingo Septemba 19 katika nyumba yake jijini Nairobi.

Baada ya uchunguzi wa wiki tatu, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Kenya Noordin Haji ameagiza wawili hao kufikishwa Mahakama Kuu mara moja na kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

“Baada ya kupitia ushahidi uliokuwepo kwa kina nimejiridhisha kuwa unajitosheleza kuendesha mashtaka ya jinai kwa kosa la mauaji kinyume cha kifungu cha 203 na 204 cha Kanuni ya Adhabu,” ameeleza haji katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Irungu maarufu kama Jowie inasemekana alikuwa na mahusiano na Bi Kimani na yadaiwa kuwa walikutana kabla ya tukio hilo la mauaji.

Mwili wa marehemu ulibainiwa na kaka yake George bafuni huku ukiwa mikono imefungwa na kamba na shingo ikiwa imekatwa na kitu chenye ncha kali. Bi Kimani alizikwa Septemba 29 huku familia yake ikiomba haki itendeke na wahusika wachukuliwe hatua.

Polisi wamehoji watu 15 wakiwemo washukiwa hao wawili juu ya mkasa huo wa mauaji. Jowie awali alidai kuwa alipigwa risasi saa chache baada ya mauaji ya Kimani.

Hatahivyo, wapelelezi wamebaini kuwa Jowie alijipiga risasi chumbani kwa Maribe. Haijafahamika bado iwapo Jowie alitaka kujitoa uhai ama alitaka kupoteza ushahidi katika mkasa uliomfika bi Kimani.

Awali ilidhaniwa kuwa Jowie ndiye angekumbana na shtaka kuu la mauji na Maribe angeshtakiwa kwa kutoa usaidizi, lakini yaonekana waendesha mashtaka wanataka kuiachia mahakama mamlaka ya kuamua ni kwa kiwango gani wawili hao walishiriki ama hawakushiriki katika tuhuma hizo zinazowakabili.

Polisi wanashuku kuwa mauji hayo yamechochewa na masuala ya fedha.

Wapelelezi walibaini kuwa Jowie alitumia silaha ya Brian Kassaine kujidhuru.

Kissaine ni rafiki na jirani wa Maribe na Jowie, awali nae aliwekwa kizuizini lakini inaarifiwa kuwa atapanda kizimbani akiwa kama shahidi wa upande wa mashtaka.

Maribe alikamatwa na kuwekwa kizuizini Septemba 30 huku Jowie akishikiliwa siku tano kabla yake. Jowie ni mlinzi kwenye kampuni binafsi katika nchi ya Falme za Kiarabu.

Chanzo BBC