Mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa tasaf atembelea kituo kipya cha afya kianga

Mwenyekiti wa kamati  ya Uongozi wa TASSAF Unguja  Ayoub Mohamed Mahmoud  amesema kumalizika kwa  kituo cha afya  Shehia ya Kianga  Wilaya ya Magharib “B” kitatoa huduma kwa wananchi wa maeneo ya shehia hiyo na majirani.

Akizungumza na wananchi wa shehia ya Kianga  alipokuwa akikagua kituo cha afya cha shehia hiyo na kuona jinsi kinavyoendelea na ujenzi wa mradi huo amesema ni juhudi za wananchi wa shehia ya Kianga wilaya ya Magharib A .

Alisema kituo hicho kitakapomalizika tayari watumishi  wanaostahiki wataletwa wa kutosha  kwa kutoa huduma kwa wananchi wa Shehia hiyo kwa ajili ya kupata matibabu kwa lengo la kuondoshewa usumbufu .

“Kituo kitakapomalizika msiwe na wasiwasi tayari wafanyakazi watakuwepo kwa kufanya kazi hiyo na ufanisi zaidi ili kuona wananchi wanapata huduma hiyo kwa urahisi”.Alisema Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini Magharib.

Pia alisema mashirikiano ya Serikali zote mbili ikiwemo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa inaboresha Vituo vya Afya kwa kuwasogezea karibu na wanamoishi  ili  wananchi waweze kufaidika na huduma hiyo mjini na vijijini bila ya usumbufu.

Nae sheha wa Shehia ya Kianga Juma Issa Juma alisema wanashukuru  kupata mradi wa TASSAF  kwa kuwapatia  kituo hicho cha  Afya ambacho kitakapomalizika  tutafaidika kwa kupata huduma hii kwa urahisi zaidi.

Muonekano wa Kituo kipya cha Afya cha kijiji cha Kianga Wilaya ya Magharib ‘A’ Unguja ambacho kiko katika hatua za mwisho kumalizika.

Alisema wananchi wa Kianga watafaidika kwa asilimia mia moja kwani ugonjwa hauna muda maalum lakini kituo kipo hapa madaktari watakuwepo tutakuwa wenye kufaidika na matunda ya nchi yetu kwa kupitia viongozi wetu wa nchi.

Vile vile sambamba na hayo mwananchi wa shehia hiyo Subira Mohamed Jecha  amesema kwa sasa tumo furahani wananchi sote hasa  akinamama kwani kutatupunguzia masafa marefu ya kufatia huduma hiyo ya Afya  tukiwa na watoto au wajawazito kwani huduma hii tunaifata Mwera au Kizimbani.