NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Zanzibar Ndugu Othman Ally Maulid akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ofisi rasmi katika hafla iliyofanyika leo katika Afisi Kuu ya Wazazi Kikwajuni Unguja.

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Ndugu Othman Ally Maulid amesema atasimamia kwa vitendo ibara ya Tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo jipya la mwaka 2017 inayoelekeza kuwa Ushindi wa CCM ni lazima kwa kila Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Chaguzi ndogo ndogo na Uchaguzi Mkuu.

Kauli hiyo ameitoa leo katika Hafla ya makabidhiano ya Ofisi baina yake na Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Mhe. Najma Giga huko katika Afisi ya Wazazi iliyopo Mpirani Kikwajuni Zanzibar.

Ndugu Othman amesema kwamba pamoja na majukumu mbali mbali ya kiutendaji yanayoikabili Jumuiya hiyo bado ana jukumu la msingi la kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinashinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Ameeleza kuwa kila Taasisi nchini ina malengo yake hivyo kwa upande wa CCM ambayo ni taasisi ya Kisiasa ni lazima iwekeze mipango yake katika kuhakikisha inashinda na kuendelea kuongoza wananchi kwa misingi ya uadilifu.

Katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo ameahidi kushirikiana na Watendaji, Viongozi na Wanachama wote wa Jumuiya na Chama kwa ujumla ili kuleta ufanisi wa kiutendaji ndani ya Jumuiya hiyo.

Aidha amewasisitiza viongozi na watendaji wa Jumuiya hiyo kuvitumia vyombo vya Habari nchini kutangaza miradi mbali mbali inayotekelezwa na Serikali chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Dkt.John Pombe Magufuli.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo amesema atatumia miongozo mbali mbali ya CCM na Jumuiya ya Wazazi kubuni mipango mbali mbali ya maendeleo itakayosaidia kuleta ufanisi.

Naye Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Wazazi Najma Giga, amewashukru viongozi na watendaji wote wa jumuiya ya wazazi kwa ushirikiano waliompa wakati wote alipokuwa kiongozi wa Taasisi hiyo.

Aliwasisitiza Watendaji wa Taasisi hiyo kushirikiana vizuri na Naibu Katibu mpya ili kuendeleza mafanikio yaliyopo ndani ya Jumuiya hiyo.

Aidha ameeleza kuwa licha ya kumaliza muda wake wa kiuongozi ndani ya Jumuiya hiyo bado ataendelea kuwa karibu katika kushiriki masuala mbali mbali ya kimaendeleo ndani ya Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya hiyo.

Akitoa shukrani Mkuu wa Utawala msaidizi Ndugu Mustafa Rashid, amesema kwa niaba ya watendaji wenzake watafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Naibu Katibu Mkuu huyo ili kufikia malengo endelevu yaliyowekwa na jumuiya hiyo katika kuimarika kisiasa, kiuchumi na kijamii.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.