Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabulla amefanya ziara katika kisiwa cha Zanzibar na kujionea Ujenzi wa mji wa kisasa wa nyumba za kimaendeleo katika eneo la Fumba wakati wa kukabidhi nyumba 60 kwa wanunuzi wa awali.

Ujenzi wa mji huu wa kisasa wa nyumba za kimaendeleo ni mafanikio makubwa ya ujenzi wa nyumba zilizo bora, zinazozingatia mahitaji muhimu ya familia pamoja na kuzijenga kwa mpangilio maalum.

Mradi wa nyumba za Fumba ni mojawapo wa miradi mikubwa iliyoidhinishwa ambao utakuwa na nyumba 1,400 ambazo zinajengwa katika mfumo wa nyumba za chini na nyumba za ghorofa moja hadi sita ambazo utekelezaji wake utakuwa katika awamu 4, na bei ya kuanzia kwa nyumba itakuwa shilingi milioni 37 tu.

Akiongeza wakati wa ziara hiyo, Mabulla amewashauri wasimamizi wa mradi huo wa Mji wa Fumba unaotekelezwa na Kampuni ya CPS Live Company Ltd kutenga maeneo ya umma ambayo yatatumiwa na wakazi wa mji huo kwa ajili ya kupumzikia, viwanja vya michezo na maeneo ya maegesho ya magari na fukwe kwa ajili ya kupunga upepo hasa ikizingatiwa Zanzibar ina mazingira mazuri ya fukwe.

Katika ziara hii Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Angeline Mabulla aliongozwa na Naibu Waziri wa ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kwa upande wa Zanzibar Mheshimiwa Khamis Juma Maalim ambaye amemueleza kwamba kwa sasa Zanzibar imechukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha suala la makazi linaimarika kwa kasi na kuweza kukuza uchumi kama ilivyoimarika kwa nchi nyingi duniani na kueleza kuwa miji mengine 14 midogo itajengwa Zanzibar.