Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, amewaagiza Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Mikoa kuwachukulia hatua kali wale wote walioanzisha vituo vya Tuition kwa kipindi hiki, kwani wanapingana na maagizo ya Serikali na kusababisha mikusanyiko itakayoleta athari ya Virusi vya Corona.

Profesa Ndalichako amewataka wanafunzi walioko majumbani kwa sasa, watambue kuwa hiyo siyo likizo bali wamerudi nyumbani kulingana na janga kubwa linaloitesa Dunia la Virusi vya Corona.

“Kuna baadhi ya sehemu baada ya kusikia watoto wako nyumbani wameanzisha tuition, nawataka wote walioanzisha tuition waache mara moja, nawaelekeza Wakurugenzi, Wakuu wa Wilaya na Mikoa,wasimamie kikamilifu maelekezo ya Serikali, msiwafumbie macho watu walioanzisha tuition kwa sababu wanapingana na maelekezo na wanakuwa ni tishio la usalama katika maeneo yenu” amesema Waziri Ndalichako.