Kitendo cha wachezaji wa Azam FC kuonekana wakiwa wameteremka katika ndege yenye nembo ya Azam kimezua gumzo takribani wiki nzima huku watu wengi wakisema Azam FC sasa imepiga hatua hadi ya kumiliki ndege.

Meneja wa Azam FC, Philipo Alando, hatimaye amefunguka juu ya suala hilo kwa kusema kuwa ndege hiyo siyo mali ya timu bali ni mali ya Makampuni ya SSB.

Azam juzi ilikwenda kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera kuvaana na Kagera Sugar ambapo ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Alando amesema kuwa watu wamezungumza mengi sana juu ya ndege hiyo lakini ukweli ni kwamba hiyo ndege siyo mali ya timu bali ni mali ya kampuni ya SSB ambayo ndiyo kampuni mama.

“Hiyo ndege haina uwezo wa kubeba timu nzima hivyo inabeba abiria 13 tu, kwa sababu ni mali ya kampuni kwa ajili ya mambo mbalimbali ya viongozi wetu, juzi ilitakuwa kuja Bukoba kwa nia ya kuwaleta baadhi ya viongozi na lengo jingine likiwa ni kurudi na baadhi ya wachezaji wa timu za taifa ili wawahi kuripoti maana tulijua kurudi na basi kwa pamoja wangeweza kuchelewa kuripoti kambini,” alisema Alando.