Nikki wa Pili ambae ni msanii wa muziki wa HipHop nchini Tanzania amefunguka na kuwashauri vijana wanaotarajia kuingia ndani ya ndoa kuwa wawe makini na wapenzi wao kabla ya kufanya maamuzi hayo.

Msanii huyo anayetamba na nyimbo zake mbili, ‘Kanifuata’ aliomshirikisha Jux pamoja na ‘Dubai’ amesema hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo amesema,

“Kabla hujafunga ndoa na mtu jaribu kuchunguza ujana wake kautumia vipi?, usije kuwa na mtu anajifunzia kwenda ‘club’ ndani ya ndoa, anatafuta ‘likes’, ndio anaanza kujua na kupata mademu, au ndio anagundua kuwa anavutia wavulana, utapata tabu sana…..maisha nikama usingizi ukikesha lazima ulale mchana…..kila steji muhimu kuipitia na mambo yake usiwe na deni”.

Miezi michache iliyopita, Nikki alimtambulisha mpenzi wake kupitia mitandao ya kijamii, ambapo aliweka picha mbalimbali zenye ujumbe wa kudhihirisha mahusiano hayo, jambo ambalo hakuwahi kulifanya kabla na kuzua gumzo kubwa.

Lakini mwenyewe alikuja kuthibitisha baadaye katika mahojiano mbalimbali kuwa mwanadada huyo ndiye mpenzi wake.