MKUU wa Wilaya ya Mkoani Pemba Hemed Suleiman Abdalla, amesema atambua jipu sheha yeyote kwenye wilaya yake, ambae atavurunda hasa baada ya mafunzo ya kisheria yaliotolewa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC hivi karibuni.

 

Alisema mafunzo yaliotolewa na Kituo hicho, ndio hasa yanayoendana na kazi za masheha hao tena kisheria, sasa amesema haoni tabu kumuwajibisha sheha, ambae atafanya majukumu yake bila ya kufuata sheria.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa tamko hilo, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya kutambulisha kazi za wasaidizi wa sheria kwa masheha na madiwani hao, yalioandaliwa na kufanyika Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC, tawi la Pemba.

Alisema katika mafunzo hayo ambayo masheha hao walijifunza sheria za tawala za mikoa, sheria ya rushwa, sheria ya maendeleo ya karafuu pamoja na kutambua kazi za wasaidizi wa sheria, ni elimu tosha ya kuwatoa masheha hao na madiwani kufanya kazi zao kwa mazoea.

“Leo (jana) masheha mmepewa mafunzo hasa yanayoendana na kazi zenu, sasa sioni sababu kufanya kazi zenu kwa mazoea, hapa sasa akitokezea sheha kuvurunda, huyo ni jipu na nitamtumbua’’,alisema.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa wilaya ya Mkoani, amekipongeza Kituo hicho kwa kuendelea kuielimisha jamii, juu ya elimu ya kisheria pamoja na kutoa msaada wa kisheria bila ya malipo.

Mapema Mratibu wa mafunzo hayo Safia Saleh Sultan, alisema mafunzo hayo kwa masheha na madiwani, ni utekelezaji wa mpango kazi wa ZLSC katika mwaka wa kazi.

Nae Mratibu wa ZLSC tawi la Pemba Fatma Khamis Hemed, alieleza kuwa wakati umefika kwa masheha na madiwani hao kukitumia kituo hicho, kwa ajili ya kujipatia elimu zaidi kupitia vitabu na machapisho yaliopo.

Baadhi ya masheha na madiwani walioshiriki mafunzo hayo, wamependekeza mafunzo mengine kama hayo, kuwajumuisha na watendaji wengine kama Jeshi la Polisi, ili kuwaeleza changamozo zao katika shehia.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalioyatayarisha na Kituo cha huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, yamejumuisha washiriki 30 ambao ni masheha na madiwani na mada kadhaa zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na sheria ya rushw   a na dhana ya wasaidizi wa sheria.

Na Haji Nassor, Pemba