Miongoni mwa changamoto kubwa ambazo zimekuwa zikizungumziwa katika Jamuhuri ya kidemokrasi ya Kongo umekuwa Ebola na mapigano ya mashariki mwa nchi.

Lakini kuna changamoto kubwa ambayo imesahaulika na kupuuzwa nayo ni ripoti zinazotolewa juu ya vifo vya wafungwa wanaokufa ndani ya magereza mbali mbali nchini humo kwa kiwango kikubwa. Katika mji wa Mbanza Ngungu takriban wafungwa 40 walizikwa mwezi machi pekee, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC wa mjini Kinshasa Emery Makumeno aliyefanya uchunguzi kwenye gereza hilo.

Jela la Mbanza Ngungu linaonekana kama lundo la matofali mekundu yaliyozeeka.

Wafungwa katika jela hilo husimama wakati wote kwenye nyuma ya vizuwizi vya vyuma wakiwa vifua wazi, anasema Makumeno. BBC haikuruhusiwa kuingia ndani wala kuchukua viedeo wala sauti yoyote ilipozuru gereza la Mbanzangungu.

Wanajeshi makumi kadhaa wenye silaha nzito nzito hulinda gereza usiku na mchana.

Joceline Bikendu, mwenye umri wa miaka 23, ambaye alifungwa mwaka mmoja kwa mashtaka ya ukatili anasema alipokuwa katika gerezani alikuwa mjamzito na anasema alikwa akilazimika kuwaomba wapita njia kitu cha kula kupitia shimo dogo lililokuwa kwenye ukuta wa gereza la Mbanza Ngungu.

Ningeweza kukaa siku nzima bila chakula. Nilikuwa nasikia mtoto akicheza tumboni nahisi kuzunguzungukabla ya kulala. Gereza lilikuwa linatupatia kiwango kidogo sana cha unga wa muhogo kupika ugali lakini hata mtoto mchanga asingeweza kushiba”.

Wahudumu wa gereza walituambia kuwa wafungwa hupata mlo mmoja kwa siku wa ugali wa muhogo kwa majani ya mihogo (kisamvu). hakuna nyama wala samaki, na senti 20 tu hutumiwa kwa gharama ya chakula cha mfungwa mmoja. Lakini kiasi hicho ni robo tu ya gharama za mfungwa kulingana na sheria.

Mara nyingi Joceline anasema wanapokosa chakula kwa mwezi mzima , ndipo wafungwa wengi hufa.