Mwendesha mashtaka wa Umma amemshitaki Rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir kwa makosa ya kuchochea na kuhusika na mauaji ya waandamanaji.

Ni baada ya uchunguzi uliofanywa kuhusu kifo cha Daktari aliyeuawa wakati wa maandamano yaliyosababisha kumalizika kwa utawala wa Bashir mwezi uliopita.

Hatma ya Bashir anayekabiliwa pia na uchunguzi juu ya madai ya wizi wa pesa na kudhamini ugaidi, haijawa wazi tangu alipokamatwa baada ya kuondolewa madarakani .

Maandamano hayo yalifanyika kwa wiki tano na shahidi mmoja anasema tarehe 17 Januari, vikosi vya usalama viliwafyatulia risasi waandamanaji na kumuua daktari aliyekuwa akiwatibu majeruhi nyumbani kwake.

Daktari huyo ni mmoja wa watu kadhaa waliouawa wakati wa maandamano ya kuipinga Serikali, yaliyoendelea pia baada ya Jeshi kuchukua madaraka Aprili 11 yakilishinikiza kukabidhi madaraka kwa raia.