Omba omba kukamatwa na Serikali pamoja na wazazi wao

Serikali yawaagiza wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi chini ya usimamizi wa Wakuu wa Mikoa kupitia kamati za ulinzi na usalama kuwakamata ombaomba pamoja na wazazi wao na washitakiwe Mahakamani chini ya Sheria ya elimu ya mwaka 1978 inayokataza utoro, na sheria ya kanuni ya adhabu kifungu cha 166, 167 na 169(a) vinavyohusu wajibu wa Wazazi na walezi kwa watoto.

Akijibu swali hilo lililoulizwa na Mbunge wa Kiembe Samaki Mh. Ibrahim Raza, lililohoji  Serikali itachukua hatua lini kuwaondoa ombaomba katika jiji la Dar es Salaam. Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa Joseph Kakunda amesema kuwa wapo ombaomba katika maeneo ya jiji la Dar es salaam kwa sababu vipo vivutio vingi ikiwemo watu wenye imani mbalimbali ambao huwapatia fedha na vitu vingine kama sehemu ya ibada.

Ameendelea kusema kuwa kuzagaa kwa ombaomba kumekua chanzo cha uchafuzi wa mazingira. Kutokana na changamoto za ombaomba mara kadhaa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Da es salaam imetekeleza hatua mbalimbali za kuwaondoa ikiwemo ya kuwakamata na kuwasafarisha makwao lakini wamekua wakirudi, mfano: September 2013 ombaomba 253 na watoto 135 walirejeshwa kwao ambapo watoto 33 walirejeshwa shuleni. Hii inadhibitisha kuwa wapo watu wazima wanaotumia watoto kuomba omba.

Aidha amewataka Watanzania kutumia fursa za kupambana na umasikini zilizoandaliwa na serikali ikiwemo Elimu msingi bila malipo, huduma za Afya vijijini na uwepo wa sheria ya fedha 2018 inayotoa fursa kwa makundi mbalimbali ya uzalishaji mali kupata mikopo wakiwemo walemavu. Vilevile watumie uwepo wa ardhi ya kutosha yenye rutuba kama fursa ya kuweza kujitegemea na hivyo kujikomboa dhidi ya kuombaomba.