Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amekanusha taarifa za kupatikana kwa mfanyabishara Mohammed Dewji, na kwamba taarifa zilizosambaa kuwa amepatikana sio sahihi.

RC Makonda ametoa onyo kali kwa yeyote atakayeibuka na kuanza kusambaza taarifa za uongo kuhusiana na tukio hilo au kuligeuza na kulifanya mtaji wa kisiasa.

Amesema msemaji wa tukio hili kwa upande wa polisi ni  Kamanda wa Kanda Maalum Dar es salaam Lazaro Mambosasa na kwa upande wa Serikali ni yeye.

Katika hatua nyingine,Makonda, amependekeza  kufungwa kwa Kamera katika maeneo yote jijini Dar es salam, ili kupata msaada mkubwa yanapotokea matukio ya kiuhalifu kama hiyo.

Amesema iwapo Dar es salaam itafungwa kamera, itakuwa msaada mkubwa kwa vyombo vya usalama kufuatilia matukio ya kiuhalifu kama la kutekwa kwa Mo Dewji.

“Tuna mpango mkubwa zaidi nafikiri umefika wakati sasa wa mkoa wa Dar es salaam wote kufungwa camera, leo hii tungekuwa na camera, tungeongezea hata weledi wa jeshi letu la Polisi kufuatilia gari iko wapi, ifike hatua Dar es salaam iwe na camera tukamate wahalifu kwa haraka zaidi, kuliko kutumia nguvu kubwa kumfuatilia mtu ambaye hujui amepita wapi”, amesema Paul Makonda.