PAZA YAWARUDISHA WATORO SHULE

Kama ilivyokuwa kwa vijiji vingi suala la elimu halijapewa kipaumbele na wananchi wa vijiji hivyo hasa katika maeneo ya ukanda wa pwani ambao watoto wengi wamekuwa wakijishirikisha na uvuaji samaki kufanya kazi za kwenda mashambani kama ukulima na uparaji samaki wakiwa na umri mdogo.

Hivyo hivyo watoto upande wa Shehia ya Mzuri kusini Unguja wamekuwa na tabia hiyo licha ya kazi kubwa inayofanywa na wana mtandao pamoja na wanaharakati kutaka wanafunzi hao kurudi shuleni na kusoma masomo yao kama kawaida.

Wanafunzi hao wengi wao wanatoa sababu kwamba wazazi wao ndio chanzo cha wao kutoroka shuleni kutokana na hali ya umasikini kwa kuwakosesha sare za shule pamoja na kuwatuma kwenye maeneo ya kupara samaki na kwenda shambani.

Lakini Mradi wa kukuza uwajibikaji Zanzibar (PAZA) umefanikiwa kupunguza matatizo mengi katika wilaya ya kusini Unguja ikiwemo tatizo la utoro na uzalilishaji wanafunzi ambapo sasa baadhi ya wanafunzi wamerejeshwa shuleni kuendelea na masomo baada ya kutoroka na kujishughulisha na mambo mengine.

Bi Zawadi Hamdu Vuai (53) mkaazi wa shehia ya Mzuri amesema utoro na vitendo vya udhalilishaji kwa wanafunzi vimepungua baada ya wananchi wakiwemo wazazi wa wanafunzi na kutakiwa kuwaruhusu watoto wao waendelee na masomo.

Mradi wa kukuza uwajibikaji Zanzibar (PAZA) unaotekelezwa  na taasisi tatu ikiwemo Chama Cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Zanzibar, Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) na Jumuiya ya Uhifadhi wa Msitu wa Ngezi Pemba (NGENARECO).

Amesema baada ya mradi wa PAZA kuwahamasisha  wananchi njia za kutatua matatizo yanayowakabili katika maeneo wanayoishi, ambapo vijana  wa shehia ya Mzuri, Nganani na Kajengwa wamechukua hatua   kufuata watoto watoro majumbani mwao na kuwapeleka skuli hali iyopelekea kupunguza utoro kwa watoto wao.

Bi Halima Mohammed Abass (37) yeye amesema kuja kwa mradi kama huu wa uwajibikaji unaaidia kuwawajibika watendaji lakini elimu inayotolewa kwa umma hasa katika vijiji kama kijiji chao  ni vizuri kwa kuwa wananchi wanaelimika.

Hata hivyo amewaomba wasimamizi wa Mradi  wa PAZA kuliangalia tatizo hilo kwa makini kwa kuwa baadhi ya wazazi wanapuuza kuhimiza watoto wao kwenda skuli na badala yake wanaona kuwatumikisha wanafunzi na ndio kuwasaidia kwa kuwa wanapata fedha za kujikimu.

“Kuna wazazi wengine huwa wanapuuza masuala ya elimu na hivyo kuwaachia watoto wao kwenda kufanya kazi za kupara samaki na kujituma kwa kazi nyengine, wazazi wa aina hiyo wanahitaji kupewa elimu ili wajue umuhimu wa elimu kwa watoto wao, kwani watoto wanaposoma watakuja kuwasaidia baadae” alisema Bi Halima.

Aidha Bi Halima alisema baadhi ya walimu hawasomeshi ipasavyo na ndio sababu wanafunzi huwa wanarudi majumbani wakiwa na baadhi yao hukatisha masomo kutokana na kuwa kuwepo kwao shule hakuwashawishi wanaendelea na masomo.

“Walimu nao wanatakiwa wahimizwe wajibu wao kwa sababu ili mwanafunzi aweze kupenda masomo ashawishiwe na mwalimu wake lakini walimu inaonesha hawatumii mbinu za usomeshaji ipasavyo” aliongeza Bi Halima.

Naye afisa elimu kusini Unguja  Haji Mohamed Abdulla (58) akijibu suali la mwandishi aliyetaka kujua mfumo wa ufundishaji wanafunzi amesema wataendelea na Uwajibikaji kwa wanafunzi kwa kutoa huduma bora  na kuhakikisha ufundishaji unafanyika kwa kufuata mtaala.

Akizungumzia kuhusu majengo ya skuli amesema ofisini yake itaendelea na utaratibu wa kusimamia majengo ya skuli kuwa safi na mazima pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika  mazingira bora na salama.

Aidha amesema hana budi kuushukuru Mradi wa PAZA kwa kuwaondolea shida ya maji katika eneo hilo kwani wananchi wameridhika kwa kupata maji safi na salama japokua yanatoka kwa mgao lakini wanaamini mradi ukiendelea maji yatapatikana yakutosha kwa wananchi wa kusini unguja.

Mradi wa kukuza Uwajibikaji Zanzibar (PAZA) ulianza mwaka jana kwa lengo la kukuza Uwajibikaji Zanzibar ili kuwahamasisha wananchi njia za kutatua matizo yanayozunguuka katika jamii na utarajiwa kumalizika  mwakani

Mradi wa Kukuza Uwajibikaji, Promote Accountability Zanzibar (PAZA) unafanya kazi katika shehia za Unguja na Pemba kwa kushirikiana na Asasi za kiraia, Halmashauri na wana mitandao na unasimamiwa na ZANSAP na kufadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya, European Union (EU)