Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo mashine za kuangalia vichochezi vya mwili (hormone) kwa watoto, vilivyokabidhiwa kwa uongozi wa wizara ya Afya.

Akikabidhi msaada huo, katika hospitali kuu ya Mnazimmoja, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Khadija Shamte, alisema PBZ ni benki ya watu hivyo wana haki ya kusaidia masuala mbalimbali yanayowagusa wananchi.

Alisema, sekta ya afya ni muhimu katika maendeleo ya nchi na bila ya afya hakuna nguvu kazi iliyo bora.

Alisema, sekta ya afya ni muhimu katika maendeleo ya nchi na inahitaji mambo mengi hivyo aliwaomba wadau wengine kuendelea kutoa misaada na vifaa mbalimbali kuisaidia  sekta hiyo muhimu ambayo inasaidia watu hasa wanyonge.

“Sekta hii ni muhimu sana katika kuboresha afya za wananchi na kurudisha nguvu kazi kwani bila ya afya hakuna kitu kinachoweza kufanyika,” alisema.

Hata hivyo, alisema PBZ sio mara ya kwanza kutoa misaada  ya aina hiyo katika sekta ya afya na kuahidi kuendelea kusaidia kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.

Hivyo, alisema ni imani yake kuwa vifaa hivyo vitasaidia wagonjwa wanaofika katika hospitali za serikali na sekta nzima ya afya.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Halima Maulid Salum, alipongeza PBZ kwa kuendelea kuwajali na kila mara kuendelea kuikumbuka jamii hasa wizara ya afya ambayo ni sekta muhimu ya maisha ya watu.

Alisema PBZ inaonyesha uzalendo ambao aliouweka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye ameipa kipaumbele sekta hiyo na kujitahidi kutoa huduma zote kuhakikisha kwamba huduma zote za afya ikiwemo vifaa tiba na dawa zinapatikana pale wananchi wanapokwenda katika hospitali zake.

PBZ ilikabidhi mashine mbili, magondoro 50 na vitanda 50 pamoja na mashuka 50 ambavyo vitu vyote hivyo vimegharimu zaidi ya shilingi milioni 85.