Mbarawa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amewataka Watendaji wakuu, Mameneja na Wazalishaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kutumia maarifa na taaluma zao ili kuboresha utendaji kazi wa wakala huo na kuongeza mapato.

Akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha TEMESA Taifa mkoani Morogoro, Prof. Mbarawa amewataka watendaji wa temesa kubadili mfumo wa utendaji na kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo na faida.

“Tengenezeni magari 60 kwa siku muone namna mtakavyopata wateja wengi na kuongeza mapato”, amesema Prof. Mbarawa.

Kikao kazi hicho chenye malengo ya kuboreshaj utendaji wa wakala huo kitajadili kwa kina changamoto mbalimbali zinazoikabili TEMESA na kutengeneza mpango wa  kuboresha huduma zao.

“Tumieni elimu mliyonayo kwa ajili ya maslahi ya watanzania na kuibadilisha TEMESA hii kuwa ya tofauti  na ya pekee”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amehimiza Wakala huo kuhakikisha wanadhibiti mapato na matumizi ya mfumo wa kielektroniki kwenye vivuko vyote ili kukuza na kujiendesha kwa vivuko vyenyewe.

Amesema mpaka sasa TEMESA ina jumla ya vivuko 27  lakini mapato yake bado yapo chini ya inavyotegemewa
na kushindwa kumudu hata matengenezo ya wakati ya vivuko hivyo.

Wakala huo pia umesisitizwa juu ya  usimamizi wa kina wa usalama wa vivuko na kanuni za usafiri wa majini ili kuepuka ajali zinazotokana na uzembe wa kutofuata kanuni na taratibu zilizowekwa.

“Andaeni kozi fupi kwa ajili ya watumishi wanaosimamia vivuko na kuja na mikakati madhubuti ya jinsi ya kuziepuka ajali ambazo zinaweza kuepukika”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Prof. MBARAWA amewataka TEMESA kutengeneza magari yote ya serikali na kutafuta soko katika magari ya watu binafsi ili kuongeza mapato na ufanisi kwa wakala huo.

“Bado mmelala, hamjaamka,  nataka temesa itengeneze magari yote ya serikali hadi kufikia asilimia 65 ya matengenezo, tumieni fursa hii ya wizara yenye taasisi nyingi ili kufanya biashara na kujilipa wenyewe na kwani inajitosheleza kukua”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Ameongeza kuwa temesa wamepewa rasiliamali zote hivyo ni lazima wafanye kazi na kujisimamia wenyewe kwa kufanya kazi kwa weledi ili kutimiza mahitaji ya watanzania.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Eng. Manase Ole Kujan amemhakikishia Waziri kuandaa mikakati madhubuti ya kuikuza wakala huo kwa kutoa huduma bora zinazolingana na thamani ya fedha yenyewe kwa wateja wake.

Katika Hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa daraja la Ruvu chini katika barabara ya Msata-Bagamoyo lenye urefu wa mita 140 na kumtaka Mkandarasi Estim Construction kuhakikisha daraja hilo linakamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.

Aidha amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Pwani Eng. Tumainieli Sarakikya kuhakikisha kipande cha barabara kilichobakia katika barabara ya Msata-Bagamoyo kinaunganishwa ifikapo Februari mwakani.

“Hakikisheni wananchi hawavamii maeneo ya hifadhi ya barabara kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na tutachukua hatua kali kwa watakaovunja sheria ya barabara”, amesisitiza Waziri Mbarawa.

Zaidi ya Shilingi Bilioni 127 zimetumika katika ujenzi wa barabara ya Msata-Bagamoyo yenye urefu wa km 63.