Raia wa Kigeni kutoka Italy aliyeshambuliwa Jana Agost 9, 2018 na watu wasiojulikana majira ya saa 10 Alfajiri akiwa nyumbani kwake  amefariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mnazimmoja.

Taarifa za awali jana zilisema Marehemu aliyejulikana kwa jina moja la Ravacious (67) Raia wa Italy alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa tofali la kichwa na watu wasiojulikana huko Matemwe wilaya ya Kaskazini A Unguja ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Mnazimmoja na taarifa zilieleza kuwa hali yake inaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Akithibitisha kufariki kwa Mgeni huyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kaskazini Unguja Haji Abdalla Haji, amesema jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuwabaini waliohusika na tukio hilo huku akiwaomba wananchi wa maeneo hayo kutoa ripoti Polisi iwapo watabaini chochote kuhusiana na tukio hilo.

Taratibu za kuusafirisha mwili wa marehemu kuelekea kwao Italy kwa mazishi teari zimeshaanza.