UONGOZI wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ umetakiwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya Kamera pamoja na manufaa ya Mradi wa Mji Salama tangu kuanzishwa kwake

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  aliyasema hayo leo, Ikulu Jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ wakati ilipowasilisha Utekelezaji wa Mpango Kazi  kwa kipindi cha Julai hadi Disemba kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa Ofisi hiyo inapaswa kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kwa kuonesha vipindi vya matukio yanayopatikana kutokana na msaada wa mradi wa Mji Salama kupitia CCTV zilizowekwa katika Jiji la Zanzibar hatua ambayo itawapelekea wananchi kuuamini kuwa mradi huo unafanya kazi ipasavyo.

Alieleza kuwa matukio hayo yakiwemo uvunjifu wa sheria iwapo yataoneshwa katika vyombo va habari ikiwemo ZBC Televisheni wananchi watapata kujua umuhimu na kazi za mradi huo kupitia CCTV zilizowekwa katika maeneo yote ya Jiji la Zanzibar hivyo itasaidia kudhibiti uhalifu..